02 September 2013

ASKARI JWTZ AMEKUFA KISHUJAA DRC- MEMBE


 Meja Khatib Mshindo
Wanajeshi wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), wakitembea kwa mwendo wa pole pole wakiwa wamebeba jeneza lenye mwili wa marehemu Meja Khatib Shaban Mshindo, aliyeuawa Goma, nchini Kongo (DRC), hivi karibuni baada ya kuwasili Zanzibar, tayari kwa mazishi yaliyofanyika jana saa 10 jioni katika Kijiji cha Fujoni, Wilaya ya Kaskazini B Unguja. Picha ndogo kushoto ikimuonesha Meja Mshindo enzi ya uhai wake.

Na Rehema Maigala

WAZIRI wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe, jana aliongoza mamia ya waombolezaji waliojitokeza kuaga mwili wa Meja Khatib Mshindo.Meja Mshindo alifariki dunia Agosti 28 mwaka huu, baada ya kuangukiwa na bomu wakati akilinda amani katika Mji wa Goma, uliopo nchini Congo (DRC).
Mwili wa Meja Mshindo uliagwa katika Viwanja vya Jeshi Lugalo, Dar es Salaam, ambapo viongozi mbalimbali wa chama, Serikali, askari na Maofisa wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), walijitokeza kutoa heshima za mwisho.Akitoa Salamu za rambirambi kwa niaba ya Serikali, Bw. Membe alisema Taifa limempoteza mtu shujaa aliyekuwa akitekeleza majukumu ya kikazi nchini DRC.
"Taifa litamkumbuka kwa ushujaa wake...alikuwa akitekeleza majukumu ya kikazi nchini DRC, Serikali haitamsahau kwa sababu alikuwa miongoni mwa mashujaa waliokufa kazini."Kifo chake kimelifanya Taifa limwage damu ya kishujaa, waliobadi hawatarudi nyuma, watakuwa na ari ya kusongambele kwa ajili ya kuwatetea wananchi wa DRC ambao wamekata tamaa ya maisha kutokana na vita ambayo inaendelea nchini humo," alisema Bw. Membe.
Aliongeza kuwa, nchi mbalimbali za Afrika zipo katika vita ambapo waathirika wakubwa ni wanawake na watoto ambao wanashindwa kufanya kazi za kujenga uchumi badala yake wanahangaika usiku na mchana.Bw. Membe alisema, Serikali imekuwa ikipeleka wanajeshi wake katika nchi hizo ili kulinda amani katika nchi hizo.
Kwa upande wake, Mkuu wa Majeshi, Jenerali Davis Mwamunyange alisema Meja Mshindo alifariki njiani wakati akipelekwa hospitali ambapo waasi wa M23, walirusha bomu ambalo lilisababisha kifo chake, kujeruhi wengine watano ambao wanaendelea na matibabu.
"JWTZ tutaendelea kumkumbuka marehemu na kuwaombea majeruhi wapone haraka na kurejea katika majukumu yao, pia tutaendelea kuwakumbuka askari wetu waliofariki kishujaa wakiitumikia nchi yao nje ya nchi," alisema.Meja Mshindo alikuwa akifanya kazi katika Kikosi cha Mizinga 83 KJ, kilichopo Kibaha, mkoani Pwani.

Ameacha watoto watatu na mjane mmoja, mwili wake umesafirishwa jana kwenda Zanzibar kwa mazishi.

1 comment:

  1. R.I.P Shujaa wetu, hapa ulipotuacha hatuta rudi nyuma mpaka ulichokuwa unapigania kifanikiwe.
    Your Tanzanian HERO.

    ReplyDelete