02 September 2013

PINDA ATAMANI MKOA WA TABORA UWE MFANO


Na Mwandishi Wetu, Igunga
WAZIRI Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, amesema angependa kuona Mkoa wa Tabora unakuwa wa mfano kwa kushirikisha vijana kwenye kazi za uzalishaji mali.Alisema mkoa huo umethubutu, umeweza na kinachosubiriwa kwa sasa ni matokeo. Bw. Pinda aliyasema hayo mwishoni mwa wiki wakati akizungumza na viongozi na wananchi wa Wilaya ya Igunga, mkoani humo
.Kabla ya kuzungumza na viongozi hao, Bw. Pinda alipokea taarifa ya Wilaya katika Kijiji cha Simbo akiwa katika ziara fupi ya kukagua miradi ya uzalishaji inayofanywa na vijana."Mnalolifanya leo si geni, mmetumia ardhi ileile ya Igunga, Mto Manonga na Bwawa la Bulenya vyote vilikuwepo, wakuu wa Wilaya na mikoa walikuwepo, lakini mbona hawakufanya chochote...ninyi mmethubutu," alisema.
Aliwataka viongozi wa Serikali wilayani humo na vyama vya siasa, washirikiane kulea vikundi hivyo bila kujali wanavikundi wanatoka chama gani na kusisitiza vikundi husika ni kiungo muhimu cha kuleta maendeleo.
Alisifia mpango wa kuanzisha kijiji cha vijana katika Wilaya ya Sikonge ambacho alikiita "Maisha plus", kwa jinsi walivyoamua kuanza maisha katika hali ya chini wakiwa wamedhamiria kujikomboa kiuchumi kupitia kazi za uzalishaji kama kilimo, ususi, uchongaji, ufugaji mifugo na nyuki.
Mapema akiwasilisha taarifa ya maendeleo ya Wilaya hiyo, Mkuu wa Wilaya, Bw. Elibariki Kingu, alisema wametenga maeneo matano yenye ukubwa wa zaidi ya hekta 250 kwa ajili ya shughuli za wajasiriamali zinazofanywa na vikundi vya vijana.
Aliitaja miradi hiyo kuwa ni ya kilimo cha umwagiliaji cha alizeti, mahindi, vitunguu, matikiti maji na mboga za majani. Miradi mingine ni kutengeneza vyombo vya nyumbani kama vile makarai, majiko na ndoo kwa kutumia vyuma chakavu pamoja na kusafirisha abiria kwa pikipiki.
Alisema Wilaya hiyo imeweka mpango mkakati wa kutumia fursa zilizopo kujenga mazingira ya upatikanaji ajira kwa vijana kupitia sekta ya kilimo baada ya kubaini kuwa, kilimo cha vitunguu kina tija kubwa kwani hakihitaji matunzo makubwa kama dawa na pembejeo nyingine.
"Zao hili halilimwi kwa wingi hapa wilayani kwa sababu watu wengi hawana ufahamu wa matokeo, pamoja na wilaya hii kuwa kame, ina udongo wenye rutuba nyingi, kuna mabwawa mawili na malambo 51 ambayo pamoja na mahitaji mengine ya maji kwa matumizi ya nyumbani na mifugo, yanaweza kusaidia katika kilimo cha vitunguu na mbogamboga," alisema.
Akizungumzia upatikanaji wa masoko, Bw. Kingu alisema bei ya vitunguu imekuwa juu wakati wote bila kujali msimu na kuna wakati inafika sh. 100,000 kwa gunia moja."Soko la vitunguu lipo kila wakati ndani na nje ya nchi, wafanyabiashara kutoka nchi jirani za Rwanda, Burundi, Uganda, Sudan Kusini na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), wamekuwa wakinunua zao hili kutoka Tanzania.
"Wiki ijayo tutakwenda Kenya kukutana na wafanyabiashara kutoka Sudan na Kenya wanaohitaji vitunguu kwa wingi." alisema.Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Profesa Elisante ole Gabriel Laizer, alisema mwaka huu wa fedha, Serikali imetenga sh. bilioni sita zikiwa ni fedha za Mfuko wa Maendeleo ya Vijana.
Alisema idadi ya vijana nchini hivi sasa imefikia 16,195,370 ambao wanapaswa kubadilisha mtazamo wa fikra zao na kujitambua kuwa wanaweza kuboresha maisha yao kwa kubainisha fursa zilizopo kwenye maeneo wanayoishi na kuangalia watazitumiaje badala ya kusubiri kazi za kuajiriwa ambazo hazipo.
Alisema ameanza mazungumzo na wenzake walioko Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) ili kupata uhakika wa fedha za vijana kutoka kwenye halmashauri.

No comments:

Post a Comment