22 August 2013

VODACOM YAZIMWAGIA TIMU VIFAA VYA MICHEZO



Na Fatuma Rashid
KAMPUNI ya Mawasiliano ya Vodacom, ambayo ni mdhamini wa Ligi Kuu Tanzania Bara, jana imekabidhi vifaa vya michezo kwa timu 14 zinazoshiriki ligi hiyo vikiwa na thamani ya sh. milioni 400.Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana Mkurugenzi wa Bodi ya Ligi Kuu, Saad Kawemba aliishukuru vodacom kwa kutekeleza majukumu yake yaliyopo katika mkataba wao na kuzitaka klabu za ligi hiyo kuheshimu chapa ya mdhamini wakati wote wa mashindano
"Ninatoa wito kwa klabu zote kutumia kama kanuni zinavyosema, pia viongozi tushirikiane kuhakikisha ligi inafanikiwa kama inavyotakiwa," alisema. Kwa upande wake Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Mawasiliano wa Vodacom, Kelvin Twissa alisema vifaa hivyo vipo tayari na anaamini timu zote zimejiandaa vya kutosha na tayari kuingia katika mtanange wa ligi hiyo."Hii ni ishara kuwa siku hadi siku, ligi yetu inazidi kuimarika na kuwa na ushindani mkubwa zaidi, hakika tunajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya soka hapa nchini," alisema.
Twissa alitoa wito kwa wadau wenye malengo ya kukuza soka nchini, kujitokeza na kuongeza udhamini katika ligi hiyo, ili kuleta tija zaidi kwani kwa kufanya hivyo pia itasaidia kukuza vipaji hapa nchini.Vifaa vilivyokabidhiwa jana ni seti za jezi mbalimbali, viatu vya mazoezi na mechi, soksi, vikinga ugoko, nguo za mazoezi na nguo za kawaida na vifaa vingine vinavyohusika katika michezo

No comments:

Post a Comment