15 August 2013

TRAFIKI FEKI ABAMBWA DAR




Trafiki feki akiwa amesimama akiwa amevalia sare za trafiki huku ameshikilia jadala lake la kazi.

  • ANA CHEO CHA SAJINI,VITABU VYA KOTOZA FAINI
  • WANANCHI WATOA USHUHUDA JINSI WANAVYOMFAHAMU

 Na Waandishi Wetu

MSEMO wa mjini mipango, umejidhihirisha wazi baada ya Jeshi la Polisi mkoani Dar es Salaam kumkamata askari bandia wa kikosi cha usalama barabarani akiwa amevalia sare za trafiki akiendelea na kazi pasipo kugundulika kwa siku kadhaa kuwa anafanya uhalifu.


Trafiki huyo bandia mwenye cheo cha sajini, (jina halikupatikana) alikamatwa na Polisi akiwa 'kazini' maeneo ya Tabata Kinyerezi akiwa amevaa sare mpya ya Askari wa Usalama Barabarani, kikoti cha kuakisi mwanga na kofia nyeupe.

Pia trafiki huyo alikuwa na jalada pamoja na kitabu cha kutoza faini (Notification) kwa madereva wanaopatikana na makosa ya kukiuka sheria za usalama barabarani.

Gazeti hili lilishuhudia trafiki huyo feki akiwa amekamatwa na Polisi na kisha kufikishwa Kituo Kikuu cha Polisi Kati, huku akijifanya amepoteza fahamu.

Mashuhuda waliozungumza na gazeti hili, walisema wanamfahamu trafiki huyo kwa muda mrefu kiasi kwamba madereva wengi wanamuogopa, kwani akikamata gari hakuna cha majadiliano kama ilivyo kwa wengine, bali anawatoza faini moja kwa moja kati ya sh. 20,000 hadi 25,000.

"Yule tunamfahamu kwa uchapaji kazi, alikuwa hataki rushwa hata kidogo, akikukamata ujue umeumia, lazima akuandikie 'notification'," alisema dereva mmoja anayemfahamu trafiki huyo kwa muda mrefu.

"Wakati wa foleni alikuwa akisimama barabarani na kuanza kuyaongoza magari, lakini alipoona imekuwa kubwa zaidi alikuwa akiondoka kwa kuhofia kujulikana," alisema shuhuda mwingine.

Mkazi mmoja wa jijini Dar es Salaam anayemfahamu trafiki huyo, alisema; "Namfahamu huyu jamaa mambo yake ni mazuri sana nyumbani kwake, hivi sio trafiki... ahaaa haiwezekani bwana."

Aliongeza kuwa; "Yule trafiki huwa anatanua sana kwenye baa na kama kulikuwa na ugeni wa viongozi hasa wa nje alikuwa akisema anawahi kwenda kulala, kwani ataamka mapema kwenda kuongoza misafara."

B a a d h i y a m a d e r e v a wanaomfahamu trafiki huyo, walisema hawaamini kama kweli mtu huyo ni trafiki feki kwani wakati mwingine alipokutana na askari wenye vyeo vidogo chini yake walimsalimia kijeshi.

Mashuhuda hao walisema trafiki huyo alikuwa akifanyakazi kwenye maeneo ya Mkuranga na wakati mwingine alionekana akiwapangia kazi vijana walio kwenye vikundi vya Polisi Jamii ambao wanasaidia kuongoza magari. Kwa mujibu wa watoa taarifa hao, vijana wa Polisi Jamii walipomkamata dereva amekiuka sheria za barabarani, walielekezwa kwa trafiki huyo ambaye bila mjadala aliwaandikia notification.

Watu waliotoa maoni kuhusu tukio hilo, walilihusisha na uzembe katika Jeshi la Polisi kiasi cha kushindwa kujitambua. "Hawa wenzetu Jeshi la Polisi hawajajitambua, haiwezekani watu washindwe kutambuana wakati wanafanyakazi pamoja na mtu huyo," alisema John Edward.

Lakini pamoja na kulishutumu Jeshi la Polisi, baadhi ya watu walionekana kufurahishwa na kitendo cha trafiki huyo feki wakisema ni mbunifu wa ajira.

"Ingawa amefanya makosa kwangu mimi naona ni mbunifu wa ajira na amelisaidia sana jeshi la Polisi kwani walikuwa wanakaribia eneo lake la kazi madereva walikuwa waangalifu sana ili kuepuka kupigwa notification," alisema Edward.

12 comments:

  1. Kweli majanga... Wanamziki wamtungie nyimbo tu trafiki feki wetu wa bongo...awe maarufu ..ameutafuta umaarufu kwa bidii yote mwacheni awe maarufu aifaidi nchi.

    ReplyDelete
  2. Jamaa ni kiboko kwa ubunifu 100% kwanza asitahili kupewa adhabu kali kwa vile amelisaidia jeshi la polisi kwa muda mrefu na kazi yake ilikuwa ya uhakika kuliko hata hao walioajiriwa Big up kamanda feki na m\Mungu atakusaidia katika majaribu hayo. Ila mazoea mabaya kwa wakati mwingine kama ni mtaji ulikuwa unatafuta si tayari ulikuwa umeshapata kwa nini usingebuni ajira nyngine bhana mdogo? ANYWAY MAJARIBU NI MTAJI

    ReplyDelete
  3. Huyu kweli ni mbunifu. Apelekwe CCP mara moja then awe polisi. Big up mkubwa

    ReplyDelete
  4. Huyu si mpumbavuwala simbunifu il yuko nyuma ya wakubwa huko juu , ww jiulize hizo nguo kapata wapi na hicho kitabu kaokota au kapewa, HiiniNchi ya Wadanganyifu Bwana mwacheni ale na WAKUBWAAAAAA.

    ReplyDelete
  5. Mie nampongeza trafiki feki huyo aliyefanya kazi nzuri kupita wale walioajiriwa kihalali na wanaishia kubambikizia watu kesi za uwongo! Yupi afadhali? Ni afadhali huyu kuliko baadhi ya matrafiki wa kituo cha MAJENGO - Mjini Moshi!!! Sisi watu wa Moshi twavumilia mengi tungeomba tuletewe huyu trafik feki atusaidie!

    ReplyDelete
  6. Ajira zimekuwa ngumu....Hongera kwa ubunifu baba!

    ReplyDelete
  7. Nampa hongera sana

    ReplyDelete
  8. dah hata mimi namkubali wala nsiyo huyo tu wapo wengi kimsingi jeshi la polisi linabidi kujipanga upya hii ni aibu ya mwaka

    ReplyDelete
  9. Tusimlaumu ajira zimekuwa ngumu.

    ReplyDelete
  10. Heko wewe trafiki feki kwani ufeki wako haupo kwani umelisaidia taifa kuokoa pale ambapo ajali ingelitokea japokuwa hukuwa kwenye ajira

    ReplyDelete
  11. serikali itambua kuwa uhaba wa ajira ndio unapelekea mambo kama haya.

    ReplyDelete
  12. Mimi nadhani tutafute kiini cha haya matatizo ya watu kujifanya Askali polisi . Askali polisi wachache wanaolitia doa jeshi zima ndo moja wapo za sababu zinazowafanya watu kujifanya Polisi. Kama mapolisi wangekuwa waaminifu , kusingekuwa na watu ambao wangejifanya polisi. Udhaifu wa baadhi ya Polisi ni mojawapo cha chanzo cha watu kufanya hivyo. maelezo tuyoyapata ni kwambo huyu bwana alikuwa anapiga faini kila kukicha na kitabu bandia. Vitabu hivyo hivyo bandia vimekuwa vikilalamikiwa na madereza kuwa fedha za makusanyo hayafiki serikalini. Kama ingekuwa kila anayekamatwa anapelekwa mahakamani huyo polisi feki asingebuni hiyo ajira. Mimi naomba Jeshi la polisi lijitazame, lijipime na pale lilipoteleza lijirekebishe kwa dhati kwa manufaa ya nchi. Sisi raia tutajuaje kama huyu trafikifeki au polisi wa doria feki tunaishia kulilaumu jeshi zima la Polisi. Kosa la kwanza si kosa bali kurudia kosa. Hivi nauliza mkuu wa kituo huwa hatembelei vituo ambavyo wamepangwa askali ao ni mkuu wa ofisi kwa kukaa oficini kwenye hewa baridi. Kama wangekuwa wanatembelea sehemu walizopangwa askari wao vitu kama hivyo visingetokea. Narudia, tujiangalie, tujipime na tujirekebishe pale tulipokosea

    ReplyDelete