07 August 2013

TFF:3 PILLARS SASA RUKSA KUCHEZA


Na Fatuma Rashid
TIMU ya 3Pillars FC ya Nigeria sasa inaruhusiwa kucheza mechi za kirafiki nchini, baada ya kupata idhini ya Shirikisho la Mpira wa Miguu la Nigeria (NFF).Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ofisa habari Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura alisema, awali waliikatalia timu hiyo kucheza mechi za kirafiki nchini kwa vile haikuwa na barua kutoka NFF.

Alisema sasa Shirikisho hilo limetoa idhini hiyo. Pia ziara yake haikuwa inaratibiwa na wakala wa mechi anayetambuliwa na Shirikisho la Kimataifa la Mpira wa Miguu (FIFA), au mwanachama wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF).
Wambura alisema klabu hiyo kutoka Jimbo la Lagos, ilipanga ziara hiyo kwa kuwasiliana na Chama cha Mpira wa Miguu cha jimbo hilo, ambacho nacho kilitakiwa kuomba idhini NFF kwa niaba ya 3Pillars.
Ofisa huyo alisema timu hiyo sasa inaweza kucheza mechi, kwani ziara hiyo sasa inaratibiwa na Chama cha Mpira wa Miguu, Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA), ambapo ni mwanachama TFF.
"Tunapenda kukumbusha kuwa watu pekee wanaotakiwa kuandaa mechi za kirafiki za kimataifa ni mawakala wa mechi wanaotambuliwa na FIFA, au wanachama wa TFF," alisema Wambura.

No comments:

Post a Comment