12 August 2013

PONDA KUPIGWA RISASI: SIRI NZITO

  • POLISI WARUKA:WAISLAMU TUNATAKA UCHUNGUZI
  • MADAKTARI MOI WAWEKA MAMBO HADHARANI
Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Nchini Shekhe Ponda Issa, akiwa katika chumba cha dharura Kitengo cha Tiba ya Mifupa (MOI) katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MHN), Dar es Salaam jana. Bw. Ponda inadaiwa alipigwa risasi begani na polisi baada ya kuhutubia kongamano mkoani Morogoro jana.



 Na Waandishi Wetu
TUKIO la Katibu wa Jumuiya ya Waislamu Tanzania, Shekhe Ponda Issa Ponda, kupigwa risasi limetawaliwa na siri nzito, kuanzia tukio lilipotokea, jinsi alivyosafirishwa kutoka Morogoro hadi jijini Dar es Salaam na baadaye kufikishwa Hospitali ya Taifa Muhimbili kwa ajili ya kupatiwa matibabu.
Uzito wa usiri wa tukio hilo unatokana na kutojulikana moja kwa moja kwa mtu aliyehusika kumpiga Shekhe Ponda risasi, hali inayoibua maswali mengi kuliko majibu

Tukio la Shekhe Ponda, la kupigwa risasi bega la kulia na kuvunja mfupa mkubwa wa bega hilo limethibitishwa na Madaktari wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa (MOI) waliomfanyia uchunguzi kupitia Ofisa Ustawi Mwandamizi wa taasisi hiyo, Mary Ochieng.
Hata hivyo, taarifa za Shekhe Ponda kupigwa risasi zimekanushwa vikali na Makao Makuu ya Jeshi la Polisi na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, ambako tukio lilitokea.
Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Ochieng, alisema Shekhe Ponda alipokelewa hospitalini hapo saa 5 asubuhi na baada ya vipimo vya madaktari imegundulika amevunjika mfupa mkubwa wa bega la kulia, ambapo risasi imeingilia mbele na kutokea nyuma.
Alisema hali yake ilikuwa inaendelea vizuri na alitarajiwa kufanyiwa upasuaji jana.
Akizungumzia hali hiyo mpwa wa shekhe Ponda Bw. Isiaka Rashid, baada ya kupata taarifa hizo walianza kufuatilia na kuamua kwenda mkoani Morogoro lakini kabla ya kufika huko waliambiwa amepelekwa Dar es Salaam. Alisema walikutana naye maeneo ya Magomeni akiwa kwenye teksi.
Alisema walimpeleka Muhimbili ambapo walitakiwa kuwa na PF3 hivyo walienda Kituo cha Polisi Salender Bridge na kupewa PF3 kisha kuendelea na taratibu zingine.
Ha b a r i z i n a e l e z a k uwa makachero wa polisi walipiga kambi Muhimbili tangu saa 11 asubuhi jana waliendelea kumsubiri hadi alipofikishwa saa 5. Aliingizwa katika chumba cha wagonjwa wa dharura saa saba mchana, huku makachero wakiwa wamejaa eneo la Muhimbili.
Habari kutoka ndani ya Polisi zilieleza kuwa Shekhe Ponda, alikuwa chini ya ulinzi, lakini isingekuwa rahisi kumfunga pingu kutokana na hali yake.
Magari ya Polisi ya Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU) yalikuwa yameegeshwa ndani ya uzio wa Kikosi cha Zima Moto eneo la Faya, yakiwa na askari waliojidhatiti kwa silaha.
TAMKO LA POLISI MAKAO MAKUU
Jeshi la Polisi Makao Makuu limewataka wananchi kuwa watulivu katika kipindi hiki wakati suala hilo la Shekhe Ponda, likishughulikiwa kisheria.
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa jana, ilieleza kuwa, kufuatia tukio hilo, timu inayoshirikisha wajumbe kutoka Jukwaa la Haki Jinai ikiongozwa na Kamishna wa Jeshi la Polisi, Issaya Mngulu, imeanza kufanya uchunguzi wa tukio hilo.
Taarifa hiyo ilieleza mazingira ya tukio hilo, kuwa juzi mchana maeneo ya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege Manispaa ya Morogoro, kulifanyika kongamano la Baraza la Idi lililoandaliwa na Umoja wa Wahadhiri wa mkoani humo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, dakika 10 kabla ya kongamano hilo kumalizika, alifika Shekhe Ponda, ambapo alizungumza kwa muda mfupi.
Taarifa hiyo ilieleza kuwa kongamano hilo lilifungwa saa 12:05, ambapo walianza kutawanyika huku baadhi ya watu wakiwa wamezingira gari dogo alilokuwa amepanda, Shekhe Ponda.
“Baada ya kutoka katika eneo hilo, Polisi walizuia gari hilo kwa mbele kwa nia ya kutaka kumkamata kutokana na kutuhumiwa kwa kosa la kutoa maneno ya uchochez

sehemu mbalimbali nchini yenye lengo la kusababisha uvunjifu wa amani,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo na kuongeza;
“Askari baada ya kutaka kumkamata, wafuasi wake walizuia asikamatwe kwa kuwarushia mawe askari.” Kufuatia purukushani hizo, askari walipiga risasi hewani kama onyo la kuwatawanya.
Taarifa hiyo ya Polisi inaeleza kuwa wakati wa vurugu hizo, wafuasi wa Shekhe Ponda walifanikiwa kumtorosha Shekhe Ponda. “Hivi sasa imethibitika Shekhe Ponda yuko katika Hospitali ya Taifa Muhimbili akitibiwa jeraha katika bega la mkono wa kulia linalodaiwa alilipata katika purukushani hizo,” ilieleza sehemu ya taarifa hizo.
POLISI MOROGORO
Kwa upande wa Jeshi la Polisi Mkoani Morogoro, limesema kuwa halijapokea taarifa yoyote ya kupigwa risasi kwa Shekhe Ponda wakati wa mhadhara uliofanyika jana kama ilivyovumishwa katika maeneo mengi nchini.
Jeshi hilo, limesema linamsaka kwa udi na uvumba mara baada ya kupewa kibali cha kumkamata kutoka Makao Makuu ya Jeshi hilo.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Faustine Shilogile, alisema kuwa ofisi yake haijapokea taarifa ya kupigwa risasi kwa mtu yeyote aliyekuwa katika mhadhara huo, zaidi ya kijana mmoja aliyesadikiwa kupigwa tofali kichwani katika mhadhara huo ambaye alifika Polisi kupatiwa PF3.
Hata hivyo, kamanda huyo alisema kuwa jeshi lake linaendelea kumsaka, Shekhe Ponda na wafuasi wake kwa kosa la kufanya vurugu na kusababisha hasara katika Hospitali ya Mkoa Morogoro, ikiwa pamoja na kuwazuia askari kufanya kazi yao.
Alisema kuwa hadi sasa kumekuwa na uzushi na utata juu ya jambo hilo katika maeneo mengi ya kuwa Shekhe Ponda, amepigwa risasi na Polisi, hali ambayo mpaka sasa hakuna ukweli juu ya jambo hilo, kwa kuwa hakuna ushahidi wa kutosha.
PROF. LIPUMBA AFUNGUKA
Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa. Ibrahim Lipumba, amelaani kitendo cha Shekhe Ponda, kupigwa risasi, huku akilituhumu Jeshi la Polisi kuwa limehusika.
Kufuatia tukio hilo, Prof. Lipumnba ameitaka Serikali kuhakikisha Shekhe Ponda anapata matibabu haraka na kufanya uchunguzi na kumfikisha kwenye vyombo vya sheria askari aliyefanya unyama huo.
Pia alielekeza lawama zake kwa Polisi, akidai kuwa lilikuwa kikwazo wakati wa kutoa PF3 ili Shekhe Ponda aweze kupata matibabu. Alidai kuwa askari waliofanya unyama huo mkoani Morogoro akamatwe mara moja na achukuliwe hatua za kutesa raia.
KAULI YA PINDA YA
PIGA TU
Prof. Lipumba alisema kupigwa risasi kwa Shekhe Ponda, kunatokana na kauli iliyotolewa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakati wa Bunge lililopita kuwa watakaokaidi kutii sheria lazima wapigwe tu.
Alisema kuwa vyombo vya dola vinahatarisha amani, hivyo alimtaka Rais Kikwete kuchukua hatua ili kunusuru nchi isiingie kwenye machafuko ya kidini.
MSIMAMO WA CHADEMA
Chama cha Demokrasia na Maendeleo CHADEMA kimelaani tukio hilo na kimesema kuwa hali hiyo ni matokeo ya kauli ya Waziri Mkuu, Pinda. Mkurugenzi wa Habari na Uenezi wa CHADEMA, John Mnyika, alisema; “Kupigwa risasi kwa Ponda ni matokeo ya kauli ya Pinda ya kuwataka polisi wapige raia wanaokaidi.”
Mnyika alisema atapeleka hoja Bungeni ya kutokuwa na imani na Waziri Pinda kutokana na matukio yanayotokea.
MSIMAMO WA WAISLAMU
Wakati huo huo, wafuasi wa Shekhe Ponda, wametoa tamko la kuitaka Serikali imchukulie hatua Polisi anayedaiwa kumpiga risasi na kuueleza umma mazingira ya tukio hilo.
Kauli hiyo ilitolewa Dar es Salaam jana katika Msikiti wa Mtambani na Amiri Mkuu wa Baraza Kuuu la Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Yusuph Kundecha, wakati akizungumza na waandishi wa habari.
Alisema wanaamini kwamba hatari ya wailsamu ipo mikononi mwa vyombo vya dola. Alisema kuanzia sasa Waislamu hawana imani tena na polisi.
Alisisitiza kuwa; “Tunataka uchunguzi wa wazi ufanyike, hatua zichukuliwe kwa askari aliyefyatua risasi na hatua hizo ziwaridhishe waislamu kinyume cha hapo watatafakari upya nini wafanye,”alisema.
Alisema kumpiga risasi ni hatua inayolenga kuwafunga mdomo waislamu pasipokujua kwamba kufanya hivyo hakuwezi kuwaziba midomo. Alisema kuwa Shekhe Ponda alikuwa anaeleza malalamiko ya waislamu na hakuwa anafanya uchochezi kama inavyodaiwa na vyombo vya dola.
Alisema matatizo ya waislamu ambayo alikuwa anaeleza siyo siri na Serikali inayafahamu muda mrefu. Alisema kuwa serikali ilikuwa na uwezo wa kumkamata Shekhe Ponda na kwenda kupata maelezo ya kutosha tofauti na ilivyofanyika.
Naye Wakili wa Shekhe Ponda, Juma Nassor, aliitaka serikali kutolipuuza jambo hilo vinginevyo nchi itaingia kwenye matatizo. Alisema kitendo walichofanyiwa Shekhe Ponda ni ujumbe mbaya kwa waislamu.
Imeandikwa na Goodluck Hongo, Gladness Theonest, Ramadhan Libenanga, Rachel Balama na Anneth Kagenda.

7 comments:

  1. serikali ya kikwete ni ya kikumaaa,mana wanatakata waislam tuanzishe mtiti na litakuja vagii si la kitoto mda c mrefu

    ReplyDelete
  2. YANAYOTOKEA MISRI HAYANA MUDA YATATOKEA TANZANIA INAPOFIKIA KIONGOZI WA SIASA ANAONEKANA WAZIWAZI AKITETEA UDINI INASHANGAZA HATA WALE WANAOITWA MAKAFIRI WAMEJISAHAU KUWA DAMU YAO ITATUMIKA KUINYWESHA TANZANIA IKUMBUKWE IWAPO KAFIRI ATAUAWA HAKUNA MSIBA,MATANGA AU KUMUUA ALIYEUA KAFIRI NCHI YA MISRI CHINI YA ABDUL NASSAR HAKUKUWA NA HUU UDINI AMBAO UMEIGAWANYA MISRI KATIKA MAPANDE MAWILI KITAKAFUATA NI VITA VYA JIHAD TUONE WANAOTUMIA UPANGA NA WANAPIGA SERA YA JICHO KWA JICHO NA JINO KWA JINO HAIPO HIVI SIJUI WANA UPAKO WA MUNGU KUWAPIGANIA KAMA SIO KUANGAMIZWA WOTE KAMA WAFIA DINI WA UGANDA KIONGOZI WA DINI ANATHUBUTU KUJINADI KUWA JINI YAKE NDIO ITAMPELEKA IKULU AMEJIDANGANYA NI VEMA AACHE MARA MOJA NI BORA AINGIE KWENYE NYUMBA YA IBADA AKASALISHE ASITUZENGUE ILA ONYO KWA WANAOITWA MAKAFIRI MUTAJIFUTA KWENYE USA WA DUNIA IKIZINGATIWA LENGO LA "NEW WORLD ORDER" NI KUPUNGUZA IDADI YA WATU DUNIANI IBAKIE BILIONI MOJA TU

    ReplyDelete
  3. Professor Lipumba tunajua wewe ni mfuasi wa Sheikh Ponda kwani hata alipoachiwa huru/kupewa kifungo cha nje wewe ulijumuika na wafuasi wa Ponda kwenda kumpa pole na ukanukuliwa na vyombo vya habari ukiunga mkono hoja za ponda. Kumbuka unautafuta urais 2015, labda usigombee, lakini kama utagombea basi nakushauri uachanae na mawazo hayo hutapata kitu. Umeonyesha kuegemea upande mmoja wa dini. Matukio ya kumwagiwa tindikali viongozi wa bakwata Arusha na mashehe na wageni huko Zanzibar hujajitokeza kulaani kwa nguvu namna hii. Hatutaki nchi hii isitawalikie na kupoteza misingi ya amani na dini zisitumike kuchochea uvunjifu wa amani. Vurugu zikaiza hazichagui dini, kabila wala utaifa. Angalia kinachotokea, Iraq, Syria, Afghanistan, Pakstan na kwingineko, yote hiyo nikutokana na kulipiza kisasi baina ya kundi moja na jingine kwa dhana ya kuonewa. MWENYE MACHO HAMBIWI TAZAMA.

    ReplyDelete
    Replies
    1. KIJANA ACHA KUTUMIA MIGUU AU TUMBO KUFIKIRI! HEBU ACHA CHUKI TUMIA MAKILI ULIYOTUNUKIWA NA M/MUNGU! REGARDS

      Delete
  4. serikali ya Tanzania haina dini kutegemea kuwarubuni waumini wa dini yako tu kukupigia kura kwenda ikulu ni kujidanganya mtu wa aina hiyo amefilisika kisiasa labda upanga utumike kumwingiza madarakani na wala si vinginevyo kutegemea kutawala makafiri kwa upanga hizo ni enzi za ANALOJIA SI RAHISI

    ReplyDelete
    Replies
    1. MMEISHAAMBIWA KANISANI KUWA LIPUMBA NI MDINI! ILA MASLAHI YA WAISLAMU YANAPOPIGANIWA NDIPO UDINI UNAJITOKEZA VICE VERSA IS TRUE! MWAMBIENI NA BABU YENU BR,SLAA!REGARDA!!

      Delete
  5. Sheikh Ponda ni mtanzania kama watanzania wengine. Sheikh Ponda ni mkosaji kama wakosaji wengine kama ilivyo zamani Mh. Mrema au Mchngaji Mtikila ambaye alikuwa kila kukicha alikuwa anaitukana serikali na viongozi wake. Mchungaji mtikila amewahi kustakiwa mara nyingi sana kwa kauli zake. Sheikh Ponda kama Mtikila hawako tofauti. Cha ajabu Sheikh Ponda anaonekana kama mtu si wa kawaida hadi kuipelekea Serikali kutumia fedha za walipa kodi kwa kumpeleka mahakamani kwa magani sita sita na hata helikopta. Serikali na hasa vyombo vya dola mnamkuza bure Sheikh Ponda. Kwake na kwa waumini wake anaonekana kama "HERO" shujaa. Gharama hizo mnazotumia kumlinda Ponda zitumike katika kununua hata PANADOL ambazo zimeadimika sana katika hospitali za serikali.

    ReplyDelete