Na Anneth Kagenda
SERIKALI imetakiwa kuacha kutoza kodi
kubwa kwenye milango ya kuingia na kutoka katika Hifadhi ya Taifa Serengeti
iliyopo wilayani Serengeti Mkoa wa Mara kwa madai kufanya hivyo ni kuwaumiza
wananchi wa kipato cha chini.
Wito huo ulitolewa
Dar es Salaam jana na Mbunge wa Jimbo la Serengeti, Dkt. Stephen Kebwe wakati
akizungumza na mwandishi wa habari hii katika Ukumbi Mdogo wa Bunge kwenye
Kamati za Bunge zilizoanza jana jijini hapa.
Alisema, ni muda
mwafaka kwa serikali kuliangalia upya jambo hilo kwani si vema wananchi
kuendelea kukamuliwa kwa kodi kubwa badala yake wawaachie hizo hizo
zilizokuwepo na kuhoji wafanyabiashara kutolipa kodi badala yake wanapita
kwenye milango hiyo kiujanja.
"Awali kodi ya
kupita getini kwa mwananchi mmoja ilikuwa sh. 1,500, lakini serikali
ikapandisha hadi sh. 5,000 wakati malori ilikuwa sh. 25,000 na sasa ni sh.
100,000 kwa tani tano na unatakiwa kupita katika mageti mawili;
"Hivyo kwenda na
kurudi huyu wa gari atatakiwa kulipa sh. 400,000 na ikizingatiwa Serengeti
tunategemea bidhaa nyingi za viwandani ikiwamo sukari, mabati, sementi
(saruji), nondo na vifaa vingi vya ujenzi toka Arusha. Hivyo mtu akitozwa kiasi
hicho kikubwa ataweza kuhimili hali hiyo? Ninachoweza kusema ni kwamba huu
umekuwa ni mzigo mkubwa kwa wakazi wa Serengeti,"alisema Dkt. Kebwe.
Wakati huo huo, kamati
za Bunge zilizoanza jana zinatarajiwa kupitia taarifa na mipango ya utekelezaji
katika wizara na taasisi zake na jumla ya miswada sita inatarajiwa kujadiliwa
na mingine kuitisha maoni ya wadau.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari jana na Idara ya Habari,
Elimu kwa Umma na Uhusiano wa Kimataifa ilisema kuwa vikao hivyo vitafanyika
kwa wiki mbili jijini hapa.
.
No comments:
Post a Comment