06 August 2013

MAKADA CHADEMA WAFUTIWA SHITAKA LA UGAIDI


Na Moses Mabula, Tabora
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Tabora imewafutia shtaka la ugaidi lililokuwa likiwakabili makada watano wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), hivyo kubaki wakikabiliwa na shtaka moja la kutuhumiwa kummwagia tindikali kada wa CCM, Mussa Tesha.

Akitoa uamuzi huo mjini hapa jana, Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Simon Lukelerwa, alisema amefikia uamuzi huo kutokana na shtaka hilo kutokidhi sababu za kisheria zilizotolewa na upande wa mashtaka.
Jaji huyo alisema kulingana na kifungu (C) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashtaka ya mwaka 1985, anaamuru shauri linalowakabili washtakiwa kwa sasa lihamishiwe katika Mahakama ya Wilaya ya Igunga.
Alisema sheria namba 245 kifungu kidogo (1) kinasema washtakiwa wanatakiwa katika mahakama ya sehemu ambayo wanadaiwa kutenda kosa husika.
Jaji Lukelerwa ameamuru washtakiwa wote wapelekwe wilayani Igunga kwa ajili ya kuendelea kusikilizwa upya shauri lao na kwamba dhamana ya washtakiwa hao ipo wazi iwapo watakidhi matakwa ya dhamana.
Awali ya ulinzi mahakamani hapo iliimarishwa na Polisi waliokuwa na silaha wakati kesi hiyo ikiendelea kutolewa uamuzi. Kesi hiyo ya ugaidi ilifunguliwa mahakamani hapo Juni 24, mwaka huu, baada ya washtakiwa hao kuachiwa awali wilayani Igunga, katika kesi ya madai ya kummwagia tindikali kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Tesha.
Watuhumiwa hao ni Evodius Justunian, (30) mkazi wa Bukoba, Osca Kaijage, mkazi wa Mkoa wa Shinyanga, Seif Magesa, mkazi Nyasaka Mwanza, Rajabu Daniel, mkazi wa Dodoma na Henry Kilewo.
Mapema Julai 8, mwaka huu katika Mahakama ya Hakimu Mkazi wa Mkoa wa Tabora, Hakimu wa Mahakama hiyo, Issa Ibrahim Magori, alisema alikataa kusikiliza kesi hiyo kutokana na kutokuwa na mamlaka hiyo, ambapo iliahirishwa.
Wakili wa upande wa utetezi katika kesi hiyo, Peter Kibatala, aliwaambia waandishi wa habari mjini hapa kwamba, Mahakama Kuu imetenda haki na ana imani kubwa na mahakama hiyo.
Alisema kwa kuwa washtakiwa h a o wa l i k ama twa k a t i k a sehemu tofauti hivyo kesi zao zilipaswa kusikilizwa maeneo waliyokamatiwa.

No comments:

Post a Comment