Baadhi ya wakazi wa Mivinjeni Kurasini wakiwa na bango kando ya Barabara ya Kilwa, Dar es Salaam jana, lenye ujumbe wa malalamiko ya kudai kulipwa hundi za fidia ili kupisha mradi wa ujenzi wa bandari kavu kwenye eneo hilo.
Na Waandishi Wetu
WAKAZI wa Mivinjeni Kata ya Kurasini
wilayani Temeke jijini Dar es Salaam wanaotakiwa kuhama makazi yao ili kupisha mradi wa Mamlaka ya EPZ,
wamefunga barabara ili kuishinikiza Serikali kuwalipa hundi zao na si viwanja.
Hali hiyo
ilijitokeza jana wilayani humo, saa tano asubuhi ambapo wananchi walijipanga
barabarani na kuzuia magari kupita, kwa madai wanaitaka Serikali iwalipe fidia
zao ili waweze kuondoka katika eneo hilo.
Akizungumza na
gazeti hili, Katibu anayefuatilia malipo ya wakazi hao, Judith George alisema
kuwa wakazi hao wamelala barabarani kutokana na Serikali kuwapiga kuwazungusha
pindi wanapotaka kulipwa hundi za nyumba zao ili waweze kuhama.
Alisema kuwa,
viongozi wa Serikali pamoja na EPZ walifika katika eneo hilo
Machi 13, mwaka huu na kufanya mkutano na wananchi kuhusu uwekezaji katika eneo
hilo.
Alisema kuwa,
mwekezaji alipozungumza nao walikubali kuhama ili kupisha ujenzi wa kiwanda
katika eneo hilo
la Mivinjeni na aliahidi kuwalipa fedha zao ili waweze kutafuta sehemu
nyingine.
Aliongeza kuwa,
mwekezaji huyo alifuatana na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi
Prof. Anna Tibaijuka na kuahidi wakazi hao kuwapatia viwanja mbadala katika
eneo la Kigamboni karibu na Uvumba Kibanda.
Alisema kuwa,
baada ya hapo Serikali ilishirikiana na Wilaya ya Temeke kufanya tathmini mwezi
Aprili, mwaka huu ya nyumba zote za wakazi hao na kuweka alama za kubomoa.
“Baada ya
tathmini Mkuu wa Wilaya ya Temeke, kwa kushirikiana na viongozi mbalimbali wa
Serikali na mwekezaji walifanya tena tathmini na kubaini kuna nyumba 60 zina
matatizo, eneo la Shimo la Udongo Kurasini,” alisema.
Aliongezea
kuwa, baada ya kufanyiwa tathmini walitangaziwa kwamba Agosti 26, mwaka huu
wafike wilayani kwa ajili ya kuchukua hundi zao, lakini walipofika waliambiwa
mchakato wa utoaji hundi umesitishwa.
Hata hivyo, alisema kama mc h a k a t o
wa u l i p a j i wa fidia umesitishwa kwa nini h awak u t a n g a z iwa k ama
walivyofanya mikutano mara ya kwanza ya kuambiwa eneo hilo linahitajika na
mwekezaji.
Naye mkazi mwingine wa eneo hilo, Mgeni Juma alisema
Serikali imejaa porojo nyingi kutokana na mwekezaji kutoa fedha za kulipwa,
lakini wao wanasitisha bila kutoa taarifa kwa wananchi.
Naye Rodi Panjo, mkazi wa Kurasini
alisema, walipotangaziwa hundi zitaanza kutolewa Agosti 26, mwaka huu alisafiri
kutoka Mbeya kuja kuchukua hundi yake, lakini alipofika alikuta mchakato huo
umesitishwa.
“Na ukizingatia nalala nyumba za
wageni, fedha ya kulipa nitapata wapi,” alihoji mkazi huyo.
Mkazi mwingine Gerad Mahinya alisema,
biashara zao zimefungwa kutokana na nyumba hizo kuwekwa alama ya ‘X’ hali
ambayo inawafanya wasijue hatima yao
ya maisha.
“Wakazi wengi wameshahama kutoka maeneo
hayo na wengine walikopa kutoka benki mbalimbali na kutafuta maeneo mengine ya
kukaa, huku wakitegemea kupata fedha zao ili kulipa madeni,” alisema.
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi
Temeke, Engelbert Kiondo aliwataka wakazi hao kuwa na subira na kufika Ofisi ya
Mkuu wa Wilaya saa nane jana ili kupata majibu ni lini watapewa hundi zao.
Hata hivyo, aliwataka wakazi hao kuwa
wavumilivu na kuachia magari yaweze kupita ili Alhamisi ya wiki hii, aweze
kuwasiliana na Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, aweze kwenda
kuzungumza nao katika ofisi ya Serikali ya mtaa wa Kurasini.
* Imeandikwa na Grace Ndossa, Theophil Ng’itu na Frank Monyo
No comments:
Post a Comment