BOHARI ya Dawa nchini (MSD) imetoa
mapazia mazito katika wodi ya wazazi iliyopo Hospitali ya Temeke jijini Dar es
Salaam ili kudhibiti kundi la vijana ambao wamekuwa na tabia ya kuwachungulia
mama wajawazito pindi wanapojifungua, anaripoti Mariam Mziwanda.
Akizungumza wakati wa kukabidhi mapazia
hayo jana Mkurugenzi wa Rasilimali Watu kutoka MSD, Victoria Elangwa alisema kundi
la akinamama linastahili kuthaminiwa na kuheshimiwa hivyo kuvisitiri vyumba
vyao ni muhimu hasa pale wanapohudumiwa katika uzazi.
Alisema kuwa, taasisi hiyo ya Serikali
katika kuthamini juhudi za kuboresha huduma za afya ilibaini kuwapo kwa kundi
kubwa la vijana wasiokuwa na busara, ambao huwa wanachungulia vyumba vya wodi
za uzazi na kliniki za akinamama wajawazito, hivyo kusababisha wanaohudumiwa
kuona hawana stara katika hospitali hiyo.
“Tulipata taarifa za kuwepo vijana
wasiokuwa na busara, ambao wanachungulia wodi za wanawake, kwa kupanda juu ya
malori makubwa ama kupita karibu na ukuta na madirisha, lengo lao likiwa ni
kuona wale wanaohudumiwa hasa wodi ya uzazi na kliniki na ili kukabiliana na
hali hii, MSD tumeona haraka tutandaze mapazia yenye ubora na mazito kuweza
kuwasitiri,” alisema.
Alisema kuwa, Serikali kwa kushirikiana
na washirika mbalimbali wa maendeleo wamekuwa wakiboresha huduma za jamii hivyo
ni fursa kwa kampuni na taasisi binafsi kuunga mkono kwa kuzisaidia hospitali,
vituo vya afya na zahanati ili kuweza kukabiliana na changamoto zilizopo.
Alihimiza uongozi wa hospitali hiyo
kuweza kupeleka maombi ya mahitaji MSD ya misaada ili kuongeza ushirikiano
katika kutatua kero zinazowakabili wananchi kuweza kufikia huduma bora ya afya
nchini.
Naye Meneja wa Huduma Saidizi ambaye ni
Kaimu Mganga Mkuu Hospitali ya Temeke, Dkt. Emanuel Bwana alisema, uwazi mkubwa
katika madirisha hospitalini hapo lilikuwa ni tatizo ambalo liliwafanya vijana
hao wasiokuwa na nidhamu kuchungulia mama wajawazito.
“ Tu n a s h u k u r u t a t i z o la kusitirika
akinamama wanaopatiwa huduma ya uzazi ilikuwa ni changamoto kutokana na
kudhalilishwa na vijana wasiokuwa na nidhamu, ambao walikuwa wanatumia mwanya
kuwachungulia, lakini bado kuna changamoto nyingi ikiwemo ya ongezeko la
wagonjwa hasa majeruhi wa ajali hospitalini hapa,” alisema Daktari huyo
No comments:
Post a Comment