28 August 2013

MGOMO WA WAFANYAKAZI TAZARA HALI TETE Anneth Kagenda na Salma Mzee
WAFANYAKAZI wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA), wamesema kama Serikali italazimisha treni hiyo iendelee na safari zake, wasilaumiwe kwa lolote ambalo linaweza kutokea kwa abiria wanaosafiri
.Tahadhari hiyo imetolewa Dar es Salaam jana na wafanyakazi wa mamlaka hiyo wakati wakizungumza na gazeti hili katika Ofisi za TAZARA na kudai mgomo wao uko pale pale hadi uongozi utakapowalipa mishahara yao ya miezi minne
 Walidai kushangazwa na kauli za viongozi mbalimbali wanaosema mgomo huo si halali wengine wakichanganya masilahi ya wafanyakazi hao na siasa.Walisema kitendo cha kupelekewa askari katika ofisi hizo ili wapigwe mabomu, hakiwezi kumaliza tatizo lililopo; hivyo wataendelea kukaa eneo hilo kwani hawapo tayari kuendelea na kazi bila kulipwa stahiki zao.
"Tutaendelea kugoma hadi kieleweke...tunamtaka Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda aje kusikiliza madai yetu...kama Serikali italazimisha tusafiri kabla hatujalipwa stahiki zetu, lolote linaweza kutokea tukiwa safarini," alisema mmoja wa wafanyakazi hao (jina tunalihifadhi).
Alisema uongozi wa TAZARA umekuwa ukiwatumikisha bila kujali kama wafanyakazi wanafamilia ambazo zinahitaji huduma, kulipia pango la nyumba, ada za watoto wao na huduma nyingine za msingi kama chakula.Bi. Theresia Mahagatile, ambaye alidai kupewa barua ya kusimamishwa kazi na uongozi wa mamlaka hiyo, alisema kitendo hicho ni unyanyasaji mkubwa kwani alichokuwa akikidai ni haki yake ya msingi kama mfanyakazi.
"Kimsingi sijatendewa haki kwa kupewa barua bila kuangalia upande wa pili...naungana na wafanyakazi wenzangu kusema hatuondoki hapa TAZARA hadi tulipwe," alisema.Wafanyakazi hao walikusanyika na kuimba nyimbo za mshikamano ambapo mgomo huo ulianza wiki iliyopita wakidai mishahara ya miezi minne.

No comments:

Post a Comment