28 August 2013

CUF YALAANI UCHOMAJI MAKANISA



Na Rehema Mohamed
CHAMA Cha Wananchi (CUF) kinasikitishwa na tukio la kuchomwa moto kwa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Usharika wa Segerea Wilaya ya Ilala, jijini Dar es Salaam.Pia chama hicho kimelitaka Jeshi la Polisi na mamlaka za usalama wa taifa kupambana na matukio hayo. Tukio hilo lilitokea usiku wa kuamkia Jumamosi Agosti 24, 2013.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa katika vyombo vya habari Dar es Salaam jana,imeeleza kuwa haiwezekani taifa linakumbwa na matukio ya kushambuliwa nyumba za ibada na hatua thabiti za vyombo vya dola hazionekani.
Ilieleza kuwa raia wanaofanya vitendo vya namna hiyo wamo miongoni mwetu na wasiolitakia mema taifa hivyo ni wajibu wa vyombo vya dola kubaini matukio hayo kama yanafanywa na mtu mmoja mmoja, vikundi vidogo au ni mitandao mibaya yenye lengo la kujenga chuki na uhasama baina ya Watanzania wenye dini na madhehebu mbalimbali.
Ilieleza kuwa, kama uhalifu huu unafanywa na mitandao, vyombo vya dola vinawajibika kujua mwanzo na mwisho wa mitandao hiyo, wafadhili wake na malengo yao."Pamoja na vyombo vya dola kuliita tukio hili kuwa ni 'jaribio la kihalifu,' CUF inaona kuwa huu ni mwendelezo wa mashambulizi dhidi ya nyumba za ibada na hujuma dhidi ya raia wasio na hatia na Jeshi la Polisi liwatafute wahusika kokote waliko na kuhakikisha sheria inachukua mkondo wake," ilieleza. Ilibainisha kuwa, CUF inaungana na Watanzania wote wenye mapenzi mema na nchi yao na wanaopinga vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi kulaani vikali tukio hilo

No comments:

Post a Comment