28 August 2013

WAWILI TFF WAWEKEWA PINGAMIZI



.  Na Amina Athumani

WAGOMBEA wawili wa nafasi ya urais na Kamati ya Utendaji walioomba kuwania uongozi kwenye uchaguzi wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), wamewekewa pingamizi kuwania nafasi hizo katika uchaguzi huo utakaofanyika Oktoba 27, mwaka huu.
Akizungumza Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa TFF, Boniface Wambura alisema waliopingwa ni Wallace Karia anayeomba kupitishwa kuwania urais na Vedastus Lufano anayewania ujumbe wa Kamati ya Utendaji kupitia Kanda Namba Mbili, ambayo ni Mikoa ya Mara na Mwanza.

Alisema aliyempinga Karia ni Shamsi Kazumari wa Dar es Salaam, wakati Lufano anapingwa wa Samwel Nyalla wa Mwanza.Wambura alisema pamoja na mambo mengine, Kazumari anampinga Karia kwa madai kuwa akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya Ligi, aliwashawishi wajumbe wenzake kuingia mkataba na Azam TV wakati akijua kamati hiyo ni ya muda, hivyo haina nguvu kisheria kusaini mkataba huo.

Alisema naye Nyalla, ambaye pia ni mmoja wa wanamichezo waliojitokeza kuwania ujumbe kupitia Kanda hiyo anampinga, Lufano kwa madai hana uzoefu wa miaka mitano katika uongozi wa mpira wa miguu.

Wambura alisema Kamati ya Uchaguzi ya TFF chini ya Mwenyekiti wake, Hamidu Mbezeleni itakutana leo saa 4 asubuhi kusikiliza pingamizi hizo ambapo wawekaji pingamizi na waliopingwa wanatakiwa kufika wenyewe ndani ya muda kwa vile uwakilishi hautakiwi

No comments:

Post a Comment