30 July 2013

UFADHILI KAMPENI ZA UCHAGUZI UNAKUZA RUSHWA



 Na Anne Kiruku, EANA
KUKOSEKANA utashi wa kisiasa kwenye vita dhidi ya rushwa katika Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kunatokana na jinsi kampeni za uchauguzi wa kisiasa zinavyofadhiliwa. Hayo yalibainishwa katika mkutano wa kanda uliofanyika mjini Kigali, Rwanda hivi karibuni. Imeelezwa kwamba ufadhili huo umechochea upendeleo katika uteuzi wa nafasi mbalimbali za umma,utoaji wa tenda na mikataba mingine ya huduma katika jamii.

Washirika wa mkutano huo wamewataka viongozi wa EAC waongoze vita dhidi ya rushwa kwa kusimamia ipasavyo utawala bora na kuzingatia uwajibikaji, uwazi na utawala wa sheria na sio maneno tupu bila vitendo. Mkutano hu pia umependekeza kuoanisha sheria zinazohusu vita dhidi ya rushwa katika kanda hiyo na kujumuisha kipengele cha uwajibikaji wa kisiasa.
Ili kulifikia lengo la kuwa na Afrika Mashariki yenye mafanikio na umoja wa kisiasa, wadau wote wanatakiwa kuzingatia utaratibu wa uwazi na uwajibikaji. Mkutano wa Nne wa Mwaka wa EAC juu ya utawala bora umewaleta pamoja wajumbe kutoka serikali za nchi wanachama na wadau binafsi wanaojihusisha na masuala ya kukuza utawala bora.
Mkutano huo ulioandaliwa na EAC umetoa jukwaa la majadiliano ya mambo muhimu yanayohusu utawala bora yanayogusa mwenendo mzima wa mtangamano wa jumuiya.Washiriki walibadilishana uzoefu na kupanga njia nzuri ya kukuza utawala bora na mtangamano wa kanda.
Wakati wa ufunguzi wa mkutano huo, Spika wa Bunge la Rwanda, Rose Mukantabana alikiri kwamba rushwa ni ''kansa kwa maendeleo ya kiuchumi.'' Alirudia kwamba rushwa inakandamiza demokrasia na kubeza utawala wa sheria.

No comments:

Post a Comment