04 July 2013

SERIKALI: GESI MTWARA ITAKUA DAR 2014


 Na Penina Malundo
WAZIRI wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, amesema ifikapo Julai 2014, mradi wa kulaza bomba la gesi umbali wa kilomita 534, kutoka Mtwara hadi Dar es Salaam, utakuwa umekamilika.
Alisema bomba hilo likifika Dar es Salaam, litasambazwa katika mikoa mbalimbali nchini ili Watanzania wengi ambao hawana umeme waweze kuipata nishati hiyo hasa maeneo ya vijijini.Profesa Nuhongo alisema hayo Dar es Salaam jana katika kongamano la wazi ambalo lilikuwa likijadili na kupokea maoni mbalimbali kutoka kwa wadau wa nishati juu ya miradi mikubwa ya kitaifa kwenye sekta ya nishati na madini.
"Naamini mradi huu ukikamilika, utaweza kuwanufaisha Watanzania wengi hasa waishio vijijini kupata umeme wa uhakika... hatutaangalia wingi wa vijiji mikoani bali tutaangalia wingi wa watu," alisema Prof. Muhongo.
Aliongeza kuwa, kuna tetesi zinazodai Wachina ndio wahusika wa kusambaza bomba hilo jambo ambalo halina ukweli, bali Serikali ya nchi hiyo imeikopesha Tanzania dola za Marekani bilioni 1.2 ambapo deni hilo linatarajiwa kuisha ndani ya miezi 18.
"Mradi huu ni wa Watanzania si Wachina kama inavyosemwa na baadhi ya watu hasa hivyo wananchi...njia mojawapo ya kuifanya nchi yetu iwe na maendeleo kiuchumi ni pamoja na gesi ambayo itatupa fursa ya kuiuza nchi jirani," alisema.
Hata hivyo, Prof. Muhongo alibainisha kipaumbele cha Serikali katika miradi ambayo itatekelezwa katika kipindi cha miaka mitano ijayo na njia saba mpya za umeme wa msongo wa juu.
Alisema njia hizo zitakuwa na umbali wa kilomita 3,000 ambapo mfumo mkuu wa kusafirishia umeme huo utaanzia katika Mikoa ya Dar es Salaam-Arusha, Singida-Arusha, Somanga- Kinyerezi pamoja na Makambako hadi Songea.
Aliongeza kuwa, awamu ya kwanza ya ujenzi wa njia ya kusafirishia umeme Kaskazini- Magharibi, itaanza katika Mikoa ya Dar es Salaam na Dodoma.
Prof. Muhongo alisema miradi hiyo itaongeza kasi ya upatikanaji umeme mijini, vijijini na kuweza kuwafikia Watanzania milioni tano sawa na asilimia 30 ya wananchi wote ifikapo 2016.
Alisema mwaka 2012-2013 Watanzania wanaotumia umeme nchini ni asilimia 21 ambapo mwaka 2005, walikuwa asilimia 10 ila kwa makisio ya haraka, mwaka 2015 watumiaji nishati hiyo wataongezeka kutoka asilimia 21 hadi 30.
Aliongeza kuwa, nchi zenye uchumi mkubwa katika Bara la Ulaya, zinategemea sana uchumi wa nishati mbadala ambao huuza katika baadhi ya nchi jirani na kuongeza pato lao kiuchumi.

1 comment:

  1. mipango mingi, utekelezaji ndio tatizo unagubikwa na ufisadi

    ReplyDelete