17 July 2013

MNYIKA AKUSANYA SAINI KUPINGA KODI YA SIMU


 Kassim Mahege na Frank Monyo
SERIKALI imetakiwa kusitisha kodi ya kumiliki laini za simu anayotozwa mwananchi kila mwezi kiasi cha 1,000, kwani ni mzigo kwa wananchi na ilipitishwa bila ridhaa ya wabunge kama ambavyo inadaiwa na Waziri wa Fedha, Dkt. William Mgimwa.
Kauli hiyo ilitolewa kwa waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana na Mbunge wa Ubungo, John Mnyika, kuhusiana na adha ambayo wananchi wameanza kuipata kwa kutozwa kodi hiyo.
Tayari mbunge huyo amezindua mpango wa kukusanya saini za wananchi wanaopinga kodi hiyo ili katika kikao cha Bunge kitakachofanyika Agosti, mwaka huu aweze kuwasilisha hoja binafsi ya kupinga kodi hiyo. Hadi sasa amesema ameshakusanya zaidi ya saini 23,500 na kwamba mkakati huo ni endelevu
.
Alisema wakati Dkt. Mgimwa akisoma hotuba ya Bajeti bungeni, alisema kodi hiyo aliifuta, lakini inashangaza kuona inatumika kwa wananchi.
Alisema kwenye hotuba yake ya bajeti kulikuwa na kipengele cha kodi za laini ya simu ya sh. 1,450, lakini baada ya wabunge kuguna, Dkt. Mgimwa alieleza kwamba kipengele hicho amekifuta.
Mnyika aliongeza kwamba baada ya bajeti kupitishwa, ndipo Dkt. Mgimwa alipopeleka jedwali la marekebisho ili kuiingiza kodi hiyo kwa sh.1,000.
"Kwa kuwa Waziri Mgimwa na Naibu wake wameviambia vyombo vya habari kuwa kodi hiyo inatokana na mawazo ya wabunge, namtaka ajitokeze ili ataje ni wabunge gani waliopendekeza kodi hiyo," alisema Mnyika.
Alifafanua kwamba siku ambayo wabunge walichangia bajeti hiyo, wabunge wa CHADEMA hawakuwepo kwani walikwenda kuomboleza msiba wa watu waliokufa kwa mlipuko wa bomu mkoani Arusha wakati wa mkutano wa kuhitimisha kampeni za uchaguzi mdogo wa madiwani katika kata nne.
Alisema wabunge waliotoa mawazo wa kupitisha kodi hiyo wengi wao walikuwa ni wa CCM mmoja upinzania (sio CHADEMA).
Alisema uzembe wa bunge usitumike kama kisingizio cha kuficha udhaifu wa Serikari katika suala hilo.
Mnyika aliwataka wananchi kuacha kulalamika kwa kuwa kulalamika si ufumbuzi wa matatizo.

1 comment:

  1. Watanzania wenzangu, naomba tujitokeze kwa wingi ili tujinusuru na huu mzigo tuliotishwa na hii serikali yetu tukufu! Kuna watu ambao hawawezi hata kununua vocha za shs. 1,000 kwa mwezi, bado serikali inattaka kuwaongezea KODI YA SHS. 1,000 kwa mwezi!!!! Tutafika? Tunataka watu waanze kutupa simu na kubakia kutegemea simu za jumuiya e.g. Kijiji, ukoo?

    ReplyDelete