Na Anneth Kagenda
HALMASHAURI ya Manispaa ya Kinondoni jijini Dar es Salaam, imetangaza
kuwa dereva yeyote mlevi akibainika amegonga taa mpya za sola zilizowekwa
barabarani licha ya kulipa faini sh. 50,000 atalazimika kuzinunua mpya.
Taa hizo ni
pamoja na zile ambazo zimewekwa jana katika Barabara ya Haile Selassie karibu
na eneo la Masaki.
Hayo yalisemwa
Dar es Salaam jana na Meya wa Manispaa hiyo, Yusuph Mwenda wakati wa hafla fupi
ya kupokea mradi wa taa 107 zenye thamani ya sh. milioni 896 kutoka kwa
Serikali ya China.
Alisema,
waharibifu wengi wa taa hizo za barabarani ni madereva walevi; hivyo hatua hizo
zikichukuliwa zitasaidia kupunguza kero hiyo.
“Lazima tufike
mahali tukubaliane kuhusu mambo ya maendeleo, hizi ni taa zimewekwa kwa ajili
ya kuwasaidia wananchi wetu, lakini utakuta dereva anaivamia na
kuigonga...hatutakubaliana nao watazilipa taa zetu mara moja,”alisema Mwenda.
Alisema,
manispaa hiyo ipo tayari kununua taa zingine kwa ajili ya kuzisambaza katika
maeneo mbalimbali hususan mitaani, hivyo wataangalia uwezekano wa kuomba
wapunguziwe bei.
Kwa upande
wake, Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Tawala za Mikoa na Serikali za
Mitaa (TAMISEMI), Alphayo Kidata alisema Serikali inaipongeza China kwa kufikia
maamuzi ya kuwasaidia wananchi kwa kuwawekea taa za sola.
“Jamani
wananchi tunaomba mzitunze taa hizo, kwani zipo kwa ajili yenu, madereva
chondechonde msizigonge kwani kufanya hivyo ni kuwakatisha tamaa wenzetu
waliotupa msaada huu, lakini ikumbukwe kwamba zinatusaidia kwenye kumwulika,”
alisema.
Balozi wa China nchini Tanzania, Lu Youging alisema,
lengo la kufanya hivyo ni kutokana na ushirikiano uliopo baina ya nchi hizo
mbili.
No comments:
Post a Comment