01 October 2012

Neno Negative lamfanya ajiue akidhani ana VVU



Na Zubeda Mazunde.

KATIKA kile kinachoonesha watu wengi hawapo tayari kupokea matokeo ya vipimo vya Virusi vya UKIMWI (VVU), mkazi wa Tegeta, jijini Dar es Salaam, Bw. Juma Hussen (18) amejiua baada ya kupima VVU na vipimo vyake kuonesha yupo Negative.


Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kinondoni, Bw. Charless Kenyela, aliwaambia waandishi wa habari jana, kuwa tukio hilo lilitokea juzi saa 7 mchana, ambapo marehemu alikunywa sumu aina ya NUVAN 500CC, akidhani kwamba kipimo kikionesha Negative maana yake ana virusi vya UKIMWI.

Alisema baada ya mtu huyo kwenda kupima afya yake hospitalini (hakuitaja jina) alipewa karatasi inayoonesha kufanya kipimo hicho cha HIV na majibu yake kuonekana yupo Negative.

Kwa mujibu wa Bw. Kinyela majibu hayo ya kuonekana Negative yalimpa hofu, kwani aliamini kuwa Negative maana yake ni kuwa na virusi vya UKIMWI, wakati si kweli.

Bw. Kenyela aliendelea kusema kuwa mtu huyo aliacha ujumbe kwenye note book yake unaosema kuwa; " Nawaaga ndugu zangu nimeamuwa kunywa sumu hii kwa sababu nimekutwa na ugonjwa huu wa virusi vya UKIMWI,  na ugonjwa huu aliyeniambukiza ni Asha."

Alisema wasamaria wema walimkuta mtu huyo akiwa hajafariki, hivyo kukimbizwa kwenye zahanati ya Mico ambapo alifariki wakati akiendelea kupatiwa matibabu.

Kwa mujibu wa Bw. Kinyela pembeni mwa mtu huyo ilikutwa note book yenye ujumbe huo na chupa ya sumu aliyokunywa.

Alisema mwili wa marehemu huyo umehifadhiwa katika Hospitali ya Mwananyamala jijini Dar.

No comments:

Post a Comment