20 July 2012

Serikali kumsaka nyoka mwenye miaka 209


Na Theonestina Juma, Bukoba

SERIKALI imedhamiria kumsaka nyoka mwenye umri wa miaka 209 aliyepo katika Msitu wa Akiba Minziro, uliopo Wilaya ya Misenyi, mkoani Kagera.

Lengo la kumsaka nyoka huyo ni kutokana na ukongwe wake hivyo kuwa kivutio kikubwa duniani hasa katika sekta ya utalii.

Mkurugenzi wa Misitu na Nyuki nchini, Dkt. Felician Kilahama, aliyasema hayo juzi wakati akizungumza na waandishi wa habari.

Alisema nyoka huyo mwenye futi 47, atapatikana baada ya mapito yake katika msitu huo kuonekana ila ni vigumu kuonekana hadharani kwa sababu hupendelea kuishi mapangoni.

“Huyu nyoka lazima tumfanyie mahesabu ya kumkamata kirahisi, umri wa miaka 209 sio mchezo, ameweza kutambulika Baada ya kupima urefu wa mapito yake, pia kuna chatu na nyoka wenye mapembe,” alisema Dkt. Kilahama.

Aliongeza kuwa, licha ya nyoka kuhatarisha maisha ya watafiti lazima kufanyike uharaka wa kuupandisha hadhi msitu huo uwe hifadhi ya Taifa ili kuboresha usimamizi wake.

“Kikao cha Kamati ya Ushauri cha Mkoa Kagera (RCC), kilipitisha msitu huu upandishwe hadhi, nyoka huyu ambaye ni aina ya Giant Forest Cobra, kichwa chake kina rangi nyekundu na sehemu ya kiwiliwili rangi ya kijani.

“Alianza kufanyiwa utafiti mwaka 2000 baada ya kupatikana kwa taarifa kutoka kwa wenyeji wa maeneo hayo juu ya kuwepo kwa aina ya nyoka huyo katika msitu huu,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, uongozi wa Halmashauri ya Missenyi, kupitia Maofisa wa Misitu, mwaka 2010 walianza kuweka mitego ya sindano katika mapito anayotumia ili kuchukua damu yake na kwenda kuipima vina saba ndipo ilibainika kuwa hadi kufikia mwaka huo, alikuwa na miaka zaidi ya 207.

Dkt. Kilahama alisema nyoka huyo atakuwa kivutio muhimu mkoani hapa kama atapatikana licha ya kukabiliwa na tatizo la ukumbwa wa msitu ambao hekta 25,000 kwani nyoka huyo amekuwa akihama mara kwa mara kwa ajili ya mawindo.

Ofisa Misitu wilayani hapa, Bw. Wilbard Bayona, alisema nyoka huyo ana uwezo wa kuishi siku 68 bila kula chochote zaidi ya maji baada ya kumeza mnyama yeyote ambaye atamkamata mawindoni.

6 comments:

  1. Sasa mnataka watu waanze kuabudu nyoka! atazuliwa kuwa na healing power ya kimzimu na pengine tutaambiwa ukimgusa tu nawe utaishi muda mrefu kama yeye, watu watatoka kila pembe ya dunia kuja msujudia! tumeshayaona mbona haya! huu ni mwendelezo tu! Mwacheni aendelee na miasha yake huko mwituni, msitutafutie balaa jipya

    ReplyDelete
  2. Hizo ni habari mpya na nzuri kwa wilaya mpya ya mishenyi,kwanza itachangia sana kwa nyoka huyo kuipatia wilaya hiyo watalii ambao watachangia kuongoza pato la wananchi wa wilaya ya Misenyi.Nawatia moyo watafiti hao kutokata tamaa kumtafuta nyoka huyo ambaye atakuwa kivutio kikubwa!

    ReplyDelete
  3. Nadhani kuna kitu kimekosewa kwenye hiyo habari maana kama ni Giant forest cobra (Naja melanoleuca) average height is (4.6 to 7.2 ft) na pia average life span is not more than 28 years.Sasa nafikiri kuna makosa ya kiuandishi.Nitaamini kama ingeandikwa urefu ni 4.7ft na umri ni 20.9 years.

    ReplyDelete
  4. Mmmh ft 47 na 209 yrs?? unajua urefu wa futi 47 jamani? huyo ni nyoka mkubwa sana na inakuwa rahisi kumkamata km ana futi hizo jamani uuwwiii naungana na Anonymous wa 3:30pm kutilia mashaka uandishi wa habari hii, nahisi kuna vimistake somewhere, please check tena vyanzo vyako vya habari utupe habari sahihi....Thanx.

    ReplyDelete
  5. umriumejulikana kwa kutumia mbinu gani?.

    ReplyDelete
  6. Mhh msituletee Loliondo nyingine maana serikali yetu ni wepesi wa kukimbilia mambo yasiyo na faida kwa maisha ya mwananchi wa kawaida.

    ReplyDelete