Rachel Balama na Rehema Maigala
RAIS Jakaya Kikwete, ameiagiza Mamlaka
ya Uwekezaji nchini (EPZA), kuhakikisha wananchi wanaohamishwa katika maeneo ya
uwekezaji, kuwatafutia viwanja na kuwajengea nyumba ili kuepusha migogoro
inayoweza kutokea kati ya wananchi na wawekezaji.
Alisema tatizo la wananchi kuvunjiwa maeneo yao na kulipwa fidia
ya fedha inachangia mgogoro mkubwa kwa wananchi, hivyo mamlaka husika iwajengee
nyumba na kuwawekea maeneo ambayo yatawasaidia kujiendeleza kiuchumi.
Rais Kikwete aliyasema hayo Dar es Salaam jana alipotembelea Banda
la EPZA lililopo kwenye Viwanja vya Maonesho ya Biashara ya Kimataifa
(Sabasaba).
Awali, Mkurugenzi wa EPZA, Dkt. Adelhelm Meru, alimhakikishia Rais
Kikwete kuwa miradi ya ujenzi wa viwanda na bandari umeshasainiwa, bado
utekelezaji wake.
"Kumekuwa na utaratibu wa wananchi kuvunjiwa nyumba zao na
kulipwa fidia ya fedha; hivyo kushindwa kujikwamua kiuchumi, utaratibu huu
siutaki uendelee kutumika ni vyema kila mwananchi ajengewe nyumba inayolingana na
aliyovunjiwa.
"EAPZ haina budi kuhakikisha wananchi wanapohamishwa wanapewa
viwanja, kujengewa nyumba na kuangalia kama maeneo wanayopelekwa yana fursa za
kibiashara," alisema Rais Kikwete.
Aliwashukuru
viongozi wa Mamlaka ya Maendeleo ya Biashara nchini (TANTRADE); na kuwataka
waimarishe ulinzi katika viwanja hivyo ili kuepusha madhara yanayoweza
kujitokeza wakati wowote.
Alisema
katika viwanja hayo, kunapaswa kufungwa kamera za uchunguzi ili kuepusha wi z i
u n a o e n d e l e a amb a o unahatarisha usalama wa bidhaa za wafanyabiashara
na wananchi wanaofika kupata mahitaji.
Pia Rais
Kikwete alitembelea Banda la Mamlaka ya Ufundi Stadi (VETA); na kuitaka mamlaka
hiyo ishirikiane na viwanda ili kuongeza ujuzi wa teknolojia za kisasa ambazo
kwenye baadhi ya viwanda hakuna.
Aliongeza
kuwa ni vyema teknolojia zinazotumiwa na VETA, zikasambazwa kwenye kampuni
nyingine ili iweze kuharakisha maendeleo na kukuza uchumi.
Akizungumzia
ujenzi wa nyumba za kibiashara na viwanda katika eneo la Kurasini, Dkt. Meru
alisema kuwa mradi huo ni wa ubia kati ya Serikali ya China na Tanzania.
Alisema
China itatoa fedha sh. bilioni 600 kwa ajili ya ujenzi wakati Tanzania
itagharamia ardhi na sh. bilioni 90 kwa ajili ya ulipaji wa fidia na tayari sh.
bilioni 25 zimetengwa kwa ajili ya fidia awamu ya kwanza.
Aliongeza
kuwa, mradi huo ukikamilika utatoa ajira kwa watu 25,000 ambapo Watanzania
hawatatumia fedha nyingi kwenda kununua bidhaa zao nje ya nchi bali bidhaa zote
zitapatikana nchini.
Dkt. Meru
alisema eneo la uwekezaji la Bagamoyo, mradi umetengewa sh. bilioni 50.2 na
utaanza wakati wowote.
Naye
Mkurugenzi Mkuu wa VETA, Zebadiah Moshi, alisema kwa sasa wamegundua mashine
mpya zinazotumia kelele na miale ili kuzalisha umeme kwa matumizi ya nyumbani
ambao hauna gharama kwa watumiaji.
Alisema kuwa sasa wanaendelea kuwafundisha
wanafunzi teknolojia mpya ienee kila sehemu ili kuondokana na adha ya umeme..
No comments:
Post a Comment