20 April 2011

Chuo kikuu cha kilimo kujengwa Katavi

Na Mwandishi Maalumu

MIPANGO inaandaliwa kujenga chuo kikuu kipya cha kilimo katika mkoa mpya wa Katavi katika jitihada za kuwapata wataalamu zaidi wa kilimo nchini.Waziri Mkuu
Mizengo Pinda, ambaye aliwasili kijijini kwake Kibaoni, Wilayani Mpanda juzi kwa ziara fupi ya mapumziko ya Pasaka, anatarajiwa kukutana na wadau wa ujenzi wa chuo hicho kesho, kwa mujibu wa ratiba ya ziara yake.

Kikikamilika chuo hicho kitakuwa cha kwanza katika eneo la Nyanda za Juu za Kusini Magharibi, zinazohusisha mikoa ya Rukwa na mkoa mpya wa Katavi, maeneo ambayo ni mashuhuri kwa kilimo, hasa cha mahindi.

Akiwasalimu wananchi katika Tarafa ya Inyonga, aliposimama akiwa njiani kutoka Tabora kwenda wilayani Mpanda kwa barabara, Bw. Pinda alisema anafurahi kuwa wadau wamejitokeza kujenga Chuo Kikuu Katavi wakati mkoa mpya unaanza.

Alisema mkoa wa Katavi unatarajiwa kuanza rasmi baada ya Julai Mosi wakati taratibu za bajeti yake, pamoja na ya mikoa mingine mipya iliyotangazwa kuwa itaundwa,  itakapokuwa imekwishapangwa.

Mikoa mingine mipya ni Njoluma (kwa kuunganisha Wilaya za Njombe, Ludewa na Makete), Geita (kuunganisha maeneo ya Wilaya Geita na meneo ya Kagera na Shinyanga) na Simiyu (kuunganisha maeneo ya mkoa wa Shinyanga na ya mkoa wa Mwanza).

Mapema, Waziri Mkuu alikagua ujenzi wa majengo ya Kituo cha Afya cha Tarafa ya Inyonga, kitakachokuwa na vitanda 224, maabara, vyumba vya upauaji, chumba cha maiti na nyumba 14 za watumishi,   kitakachogharimu Sh. bilioni moja na laki sita. Kituo cha Afya cha Tarafa hiyo sasa kina vitanda 25 na majengo chakavu.

Alisema Kituo hicho kitakapokamilika na Inyonga itakapokuwa Wilaya chini ya Mkoa mpya wa Katavi, kinaweza kupandishwa hadhi na kuwa Hospitali ya Wilaya.

5 comments:

  1. Kweli naishangaa sana serikali yetu. Inakuwa na mipango isiyokamilika na kuleta tija yoyote. Vyuo vya kilimo vilivyopo vinahitaji upanuzi, na vimeshindwa kutoa elimu bora sababu ya serikali kutotoa mchango wa kutosha kulingana na mahitaji. Vilevile, vyuo vyote hivyo (SUA, MATIs na LITs) havijitoshelezi wakufunzi. Badala ya kupanua hivi tulivyonavyo, tunakimbilia kuanzisha vipya. Pia wataalamu wa kufundisha na kufanya tafiti tutawatoa wapi kwa miaka hii? Na je hivi vilivyo tawanyika nchi nzima havipokei watu kutoka ukanda huo? Hili linaonekana ni la kisiasa zaidi.

    ReplyDelete
  2. Tatizo kubwa tulilonalo serikali yetu inatekeleza miradi bila kufanya utafiti wa kutosha ili kujua tatizo liko wapi na njia zipi sahihi za kutatua.
    Ukiangalia chuo kikuu chetu Cha kilimo sua kitatoa wataalam kila mwaka ila hakuna hata mtaalam mmoja wa kilimo anayekipenda au anayewekeza katika kilimo. hii inatokana na namna serikali inavyoendesha ovyo secta ya kilimo, na kuonekana kilimo hakilipi. Sasa badala ya kutafuta mikakati ya kuwafanya hawa wataalmu wa kilimo walipo wakaweza kurudisha moyo wao kalimo na kukiendeleza tunanzidi kuongeza vyuo, Hawa wa hitimu waende wapi hali kilimo hakilipi? any way,
    Tunapenda sana kuandalia inputs na outputs lakini hatuki kabisa kusikia neno impact.
    Nataka kujua impact ya chuo kikuu cha kilimo SUA iko wapi katika kuendeleza uzalishaji. zaidi kila mwaka tunasikia njaa na kupanda kwa bei za vyakula. Sijui tunakoipeleka Tanzania.

    ReplyDelete
  3. Yah, Kwa waziri mkuu!

    Ukiwa bosi unaweza kushawishi watu wa mipango.

    Bado airport na bandari zitajengwa Bagamoyo hata kama za Dar zinahitaji kupanuliwa.

    ReplyDelete
  4. Hivi Kile JK alichoahidi kujenga Musoma wakati wa kampeni mwaka jana ndiyo kimeota mbawa?

    ReplyDelete
  5. Wakumbuke wananchi wako baba Pinda maana walisahaulika. Vyuo vingine vilijengwa mahali pasipo na malighafi. Jenga Chuo Mpanda baba maana huko malighafi za mahindi zinapatikana. Ni wakati wao nao kuona nchi inavyokwenda. Tunasikia uwanja wa ndege umekwisha Mpanda na nguvu, tunasikia barabara za mji wa Mpanda zimewekewa lami. Basi hongera. Zamani tulisikia tu maendeleo mikoa mingine ya kasikazini. Hebu wasaidie watu wako nao wajione ni watanzania! HONGERA BABA PINDA!

    ReplyDelete