17 May 2013

Wanafunzi CBE, VETA, UDSM wajiuza

Na Waandishi Wetu


 WANAFUNZI wa kike wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Chuo cha Elimu ya Biashara (CBE) na Chuo cha Mamlaka ya Elimu na Ufundi Stadi (VETA), Dar es Salaam, wamefikishwa katika Mahakama ya Jiji Samora, wakidaiwa kufanya biashara ya kuuza miili yao.
Washtakiwa hao walikamatwa katika eneo la Kona Baa Ambiance, Sinza wilayani Kinondoni ambao ni miongoni mwa wanawake 35 wanaodaiwa kufanya biashara hiyo na wote walifikishwa mahakamani hapo.
Kesi hiyo ilikuwa chini ya Hakimu Willian Mtaki ambapo Mwendesha Mashtaka, Bw
. John Kijumbe, alisema wasichana hao walikamatwa katika mazingira tofauti tofauti.
Wanafunzi hao ni Yasinta Kilimo mwenye miaka 21 (CBE), mkazi wa Upanga, Morin Masatu miaka 19 (UDSM), mkazi wa Kinondoni na mwanafunzi wa VETA, aliyefahamika kwa jina moja la Khadija.
“Nilikwenda pale baa kuchukua simu yangu ambayo ilipotea hivyo waliniita nikaichukue ndipo askari wa jiji wakanikamata,” alisema Khadija wakati akijitetea.
Kwa mujibu wa Bw. Kijumbe, washtakiwa hao wamekosa dhamana baada ya kushindwa kutimiza masharti ya kila mmoja kuwa na wadhamini wawili au kulipa faini sh. 200,000.
Kesi hiyo inatarajiwa kusikilizwa tena Mei 28 mwaka huu, ambapo washtakiwa wote walipelekwa Segerea.
Wakati huo huo, Jeshi la Polisi mkoani Kinondoni, limewakamata watuhumiwa 716 waliokuwa wakijihusisha na biashara ya kuuza miili kati yao wanaume 38 na wanawake 678.
Akizungumza na waandishi wa habari jana, Kamanda wa Polisi mkoani humo, Charles Kenyela, alisema watu hao walikamatwa kwenye msako uliodumu kwa miezi sita kwenye maeneo mbalimbali ya Kinondoni.
Maeneo hayo ni baa, kumbi za starehe, madanguro, sehemu za wazi katika ufukwe wa Bahari ya Hindi na makaburini ambapo kati ya wanaume waliokamatwa, wengine ni mashoga pamoja na wateja wa machangudoa.
“Msako huu ulifanyika Maisha Club, Coco Beach, Barabara ya Tunisia, Travertine Hotel, Tandale Uwanja wa Fisi, Ambiance Club, Shekilango pamoja na Mwananyamala,” alisema.
Kamanda Kenyela aliongeza kuwa, jeshi hilo pia limewakamata raia 12 kutoka nchini Ethiopia walioingia nchini bila kibali kati ya Mei 2 na 6, mwaka huu katika eneo la Kimara Mwisho na Tegeta kibaoni.
Alisema kukamatwa kwao kulitokana na taarifa walizopata kutoka kwa raia wema waliowaona maeneo hayo.
Imeandikwa na Mosi Mrisho, Ester Maongezi na Rehema Maigala.

No comments:

Post a Comment