17 May 2013

Pinda atangaza kiama kwa viongozi


Grace Ndossa na Gladness
Theonest


 SERIKALI haitasita kuwachukulia hatua viongozi wote ambao watabainika kujihusisha na vitendo vya kuingiza na kuuza dawa za kulevya nchini.
Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, aliyasema hayo bungeni mjini Dodoma jana wakati wa maswali ya papo kwa papo. Mbunge wa Mwibara, mkoani Mara, Bw. Kangi Lugola, ambaye alidai kuwa, wapo baadhi ya mawaziri wanaojihusisha kuingiza na kuuza dawa za kulevya.
 Alisema tuhuma hizo ni nzito hivyo aliitaka Serikali iwataje kwa majina pamoja na kuchukua hatua. Akijibu swali hilo, Bw. Pinda alisema viongozi wanapitia mchujo mkali hadi kuchaguliwa kwao
hivyo kama kuna mawaziri wanaojihusisha na vitendo hivyo, majina yao yapelekwe ili washughulikiwe mara moja.

Alimtaka Bw. Lugola kuwasilisha majina na vielelezo ili majina hayo yapelekwe kwa rais na kufanyiwa kazi.
“Kauli zinazotolewa na viongozi lazima zipimwe kwanza kama hazitakuwa na madhara kwa jamii... kiongozi kabla hajazungumza lolote achuje kauli yake,” alisema.
Alisema kama Naibu Spika atamtaka Bw. Lugola atoe vielelezo itakuwa vizuri ili kujua mwisho wa jambo hilo.
Mbunge wa Viti Maalumu, Bi. Magdalena Zakayo (CHADEMA), alitaka kujua ni hatua zipi ambazo zitachukuliwa kwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dkt. Shukuru Kawambwa, kwa kuonesha udhaifu wa kuongoza Wizara hiyo.
Alisema hali hiyo inatokana na idadi kubwa ya wanafunzi waliomaliza kidato cha nne mwaka 2012 kufeli mtihani, wengine kupoteza maisha na kuhama nyumbani kwao.
Bw. Pinda alisema, tume iliyoundwa bado inaendelea na kazi yake hivyo iachwe kwanza kwani jambo hilo si dogo ila ripoti ikitoka wataangalia kama kuna haja ya kuwawajibisha viongozi.

No comments:

Post a Comment