WATU wawili
wakazi wa Kijiji cha Nyeziguni, Kata ya Magindu, Tarafa ya Kibaha, Wilaya ya
Kibaha, mkoani Pwani, wamefariki dunia na wengine saba kulazwa katika Kituo cha
Afya Chalinze, baada ya kula nyama ya mbuzi iliyokuwa imechanganywa na dawa ya
mitishamba.
Tukio hilo la
aina yake limetokea juzi baada ya watu hao kuchinja mbuzi na nyama yake kupikia
supu waliyokuwa wameichanganya na dawa ya mitishamba inayohisiwa kuwa ni sumu
ambayo imesababisha vifo hivyo.
Waliokufa
katika tukio hilo ni Kitandu Madeni (31) na Chiti Ningwa (30), waliolazwa ni
Kilendu Kobero, Balosina Tembo, Renalwa Kobero, Sokoi Sikanyi, Samso Nganyigwa,
Ole Kajikali na Yuas Juakali, ambao hali zao ni mbaya.
Taarifa
zilizopatikana eneo la tukio ambazo zimethibitishwa na Kamanda wa Polisi mkoani
Pwani, Urlich Matei, zilisema watu hao walikula nyama hiyo saa mbili asubuhi.
Ilidaiwa kuwa, jamii ya kimasai inaamini nyama ya mbuzi
ikichanganywa na mitishamba inawapa nguvu, kusisimua mwili na kuondoa maradhi
mbalimbali mwilini.
Hali hiyo ndio
iliyowafanya watu hao kufanya kitendo hicho ili wapate nguvu na kuondoa maradhi
mwilini ambapo baada ya kula supu hiyo, marehemu hao walikwenda kuchunga mifugo
yao asubuhi na kurejea nyumbani jioni.
Ilipofika saa
mbili usiku, Madeni alielekea katika eneo ambalo huoneshwa Ligi ya Uingereza
katika televisheni ambapo akiwa njiani, alianza kuharisha, kutokwa na jasho
mwilini hivyo alilazimika kurudi nyumbani haraka.
Alipofika nyumbani aliingia ndani na
kulala ambapo ilipofika saa nne usiku alifariki dunia na muda mfupi baadaye,
Ningwa alianza kuharisha, kutokwa jasho na kufariki.
Watu wengine saba ambao nao walikula
supu hiyo walianza kuharisha, kutokwa jasho lakini walikimbizwa Kituo cha Afya
Chalinze kwa matibabu zaidi.
Kamanda Matei alisikitishwa na
kitendo cha miili ya marehemu hao kuzikwa haraka kabla ya uchunguzi wa kidaktari
ili kubaini sababu ya vifo vyao.
Alikemea
tabia ya baadhi ya watu kutumia mizizi na majani ya porini bila kuthibitishwa
na wataalamu hivyo aliwataka waache tabia hiyo mara moja kwani ni hatari kwa
maisha yao.
No comments:
Post a Comment