WAZIRI Mkuu mstaafu
na Mbunge wa Monduli, mkoani Arusha, Bw. Edward Lowassa, ametoa wito wa kuwepo
mjadala mpana ambao utazungumzia tatizo la ajira kwa vijana nchini.
Bw. Lowassa aliyasema hayo Dar es Salaam jana
katika uzinduzi wa kitabu ambacho kinazungumzia na kutathmini mzozo wa kiuchumi
duniani kwa kuiangazia Tanzania.
Alisema ni muhimu wadau wote wakiwepo wasomi,
wanasiasa, wafanyabiashara na wananchi wasio na ajira hususan vijana, kushiriki
mjadala huo na kutoa mapendekezo ili tatizo hilo lipatiwe ufumbuzi.
"Nafurahishwa kuona mmoja wa wana zuoni
mashuhuri wa masuala ya
uchumi nchini, Dkt. Honest Ngowi, ametumia rasilimali
zake na muda wake kufanya utafiti.
“Ameandika kwa kina mdororo wa uchumi wa
mwaka 2008 kwa mtizamo wa Tanzania,” alisema Bw. Lowassa na kumpongeza msomi
huyo kwa kazi aliyoifanya.
Bw. Lowassa ambaye kwa muda mrefu amekuwa
akipigia kelele tatizo la ajira kwa vijana, alisema kutokana na mdororo wa
uchumi duniani mwaka 2008 na ule uliozikumba mataifa yanayotumia sarafu ya euro
mwaka 2010, tatizo la uhaba wa ajira linaweza kutatuliwa kwa kuimarisha soko la
ndani.
“Mdororo wa mwaka 2008 na 2010, ulisababisha
ongezeko la tatizo la ajira hapa kwetu...bidhaa zetu kama vile mazao na madini,
zinategemea sana soko la nje,”' alisema na kuongeza mdodoro huo kwa mujibu wa
takwimu, ulisababisha watu 48,000 kukosa ajira.
Alisema tatizo la ajira Tanzania ni kubwa kwa
uchumi wa kijamii hivyo ni bomu linalosubiri kulipuka na madhara yake ni mabaya
kwani vijana wanaweza kutumika kwa namna mbaya kwa sababu hawana cha kupoteza.
“Tukumbuke msemo unaosema kichwa kisichokuwa
na fikra yoyote basi ni karakana ya shetani," alisisitiza.
Aliwaomba wanazuoni kuongeza jitihada zao
katika kuzalisha ufahamu kutokana na tafiti zao na kwenda mbele zaidi kwa kutoa
machapisho ya tafiti zao na kuyasambaza.
Bw. Lowassa alisema sambamba na juhudi hizo,
upo umuhimu wa Serikali kuongeza ufadhili katika sekta ya utafiti, uchapishaji
na usambazaji wa ufahamu unaotokana na tafiti mbalimbali.
“Naiomba Serikali iboreshe mazingira ya uwekezaji kwa
wachapishaji na wazalishaji majarida na vitabu ili kuwa na kazi za kiwango cha
juu kutoka nchini,” alisema Bw. Lowassa na kuongeza kuwa, sekta hiyo ni moja
wapo ya mikakati mizuri ya kutoa ajira.
NCHI ZOTE ZA DUNIA HII ZINAZOENDELEA NA ZILIZOENDELEA ZILIZO NA MTIZAMO WA KUONGEZA AJIRA KWA WATU WAKE NA KUIMARISHA UCHUMI NI LAZIMA ZINATOA KIPAUMBELE KWENYE KUIMARISHA UPATIKANAJI WA UMEME WA BEI NAFUU NA USIOYUMBA; KUIMARISHA MIUNDO MBINU MAMA YA USAFIRISHAJI YAANI BARABARA,RELI,BANDARI,VIWANJA VYA NDEGE NA MIUNDOMBINU YA UPATIKANAJI MAJI AIDHA URAHISISHWAJI WA MICHAKATO YA UJASILIAMALI PIA NI MUHIMU. mheshimiwa lowassa zana anyoizungumuzia anapaswa atubu kwanza kwa kuifanya nchi kuingia kwenye mgogoro mkubwa wa upatikanaji umeme, mgogoro aliouasisi yeye mwenyewe. hili ni tatizo kubwa linalokosesha ajira kwa watu wengi kwa sasa. Mimi ninafikiri asitoe maneno ya kubutua tu apendekeze kwa maoni yake taifa lifanyeje ili kuondokana na mzimu wake wa richmond unaokosesha ajira Vijana luki. hebu fikiri welders, wafanyakazi wa saloon, selemara,wauza kanda za miziki, viwanda vidogo na vikubwa na wengine wote hawa bila umeme hawazalishi vizuri, hawapati faida ya kutosha kupanua miradi yao na bila kupanua miradi hakuna ajira mpya. sasa waziri mkuu mstaafu aseme yeye anatarajia ajira zitoke wapi kama aliua uti wa mgongo wa kutengeneza ajira.Alisha tumikia taifa kwa uwezo wake aache wengine pia watimize wajibu wao ikiwezekana warekebishe alichokosea- hana jipya
ReplyDelete