*BAJETI YAKE YAPITA, ABAINI WIZI VITUO VYA MALIPO
*AWATAKA POLISI KUZIACHIA NOAH WALIZOKAMATA
*KIGWANGALLA AIHADHARISHA CCM UCHAGUZI 2015
Goodluck Hongo na Darline Said
SERIKALI
imetoa agizo la kufungwa mara moja kwa ofisi zinazotumika kubadilisha makadirio
ya fedha ambazo hutakiwa kulipwa na wafanyabiashara katika Ofisi za Mamlaka ya
Mapato nchini (TRA), zilizopo Keko na Lumumba, Dar es Salaam.
Vituo hivyo
hutumika kubadilisha kiasi cha fedha ambacho hupaswa kulipwa TRA ili kugomboa
mizigo yao kwenye Bandari ya Dar es Salaam.
Agizo hilo
limetolewa bungeni Mjini Dodoma jana na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison
Mwakyembe, alipokuwa akijibu maswali ya wabunge wakati akihitimisha mjadala wa
makadirio ya bajeti ya
Wizara yake kwa mwaka wa fedha 2013/14.
Alisema wapo baadhi
ya watu ambao wanaitumia Bandari ya Dar es Salama kama mashine ya kutolea fedha
(ATM), na kujinufaisha wakishirikiana na baadhi ya wafanyakazi.
Aliongeza kuwa,
yeye ameingia mkataba na Rais Jakaya Kikwete ili kufanikisha malengo ya
Serikali na kama atashindwa kuyafikia malengo hayo afukuzwe hivyo hayupo tayari
kubeba lawama wakati watu wanaosababisha uzembe wanaweza kuondolewa na kupisha
wengine wafanye kazi hizo.
Dkt. Mwakyembe
alisema kwa sasa Serikali haina mzaha na mtu ambaye atakwepa kulipa kodi au
kufanya udanganyifu katika mfumo mpya wa kulipia kodi.
“Nawaonya
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bandari (TPA), Mkurugenzi Mkuu wa Fedha na
Mkurugenzi wa IT, kuanza kutumia mfumo mpya wa malipo ili kudhibiti mapato ya
bandari.
“Kama watashindwa, hatutasita kuwafukuza mara moja kwani
Bandari ya Dar es Salaam ndiyo inayotakiwa kuingiza mapato makubwa makubwa
serikalini,” alisema Dkt. Mwakyembe.
Aliwataka
wabunge na wananchi kufanya uchunguzi wa kina ndipo wahoji kwa nini Serikali
imeamua kujenga Bandari ya Bagamoyo, mkoani Pwani.
“Hatukufanya
hivi kwa sababu ya Rais Kikwete ila kutokana na hali ya kuelemewa...baada ya
miaka mitatu ijayo Bandari ya Dar es Salaam itaelemewa kwa mizigo ambayo nchi
ya Burundi inatarajia kusafirisha madini ya nikeli zaidi ya tani milioni tatu
hivyo ni lazima kuwepo na mbadala wa bandari,” alisema.
Aliongeza kuwa,
wafanyakazi wote wa Wizara hiyo lazima wafanye kazi zao kwa uadilifu ambapo
kipaumbele cha Wizara na Serikali ya awamu ya nne ni kujenga reli mpya nchi
nzima kwa ubora zaidi.
Alisema ili
aweze kutimiza malengo yake, hatamuonea huruma mtu yeyote ambaye atakwenda
kinyume na maadili ya kazi yake ndio maana anaendelea kusafisha kila sehemu.
Dkt. Mwakyembe
alisema viongozi wa Shirika la Ndege nchini, (ATCL), wameacha deni kubwa ambalo
walilipia ndege iliyokuwa kwenye matengenezo hivyo lazima kuwepo na utaratibu
wa kuwajibishana kabla ya kulirudisha katika hali ya kawaida.
“Si kwamba nchi kama Burundi au
Rwanda zinatushinda katika sekta hii bali kilichopo ni kwamba, kupanga ni
kuchagua wao wamechagua ndege na sisi tumechagua barabara,” alisema.
Akizungumzia magari aina ya Noah kubeba
abiria, aliitaka Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Usafiri Nchi Kavu na Majini
(SUMATRA), kuzungumza na watu wenye magari ili kuona uwezekano wa kufanya kazi
ya kubeba abiria kwani wote ni Watanzania ambao tunajenga nchi moja.
“Naliagiza Jeshi la Polisi kuyaachia
mara moja magari yote aina ya Noah ambayo yamekamatwa na yapo kituoni bila
masharti, watu wote wenye taarifa ya kutakiwa kulipia mizigo kwa dola badala ya
fedha za Tanzania, nileteeni majina ya watu hao ili niweze kuchukua hatua za
haraka,” alisema.
Dkt.
Kigwangalla
Katika
hatua nyingine, Mbuge wa
Nzega, mkoani Tabora, Dkt. Hamisi Kigwangalla, amekihadharisha Chama Cha
Mapinduzi (CCM), kuwa makini na Uchaguzi Mkuu wa 2015, kutokana na Mkoa huo
kuwa nyuma kimaendeleo.
Dkt. Kigwangalla aliyasema hayo
bungeni mjini Dodoma jana wakati akichangia mjadala wa bajeti ya Wizara hiyo.
Alisema Mawaziri wote wanatoka CCM
lakini anashangaa kuona Mkoa huo umesahaulika hivyo kutoa mwanya kwa wapinzani
kutumia fursa hiyo kukichafua chama chao.
Aliongeza kuwa, vyama vya upinzani
vinapokuwa katika mikutano ya hadhara huwaambia wananchi kuwa hawapati
maendeleo kutokana na kuichagua CCM hivyo lazima Mawaziri wautazame Mkoa huo
ili kujiwekea mazingira mazuri ya ushindi 2015.
“Siungi mkono bajeti ili Waziri
afanye kazi vizuri...nilisafiri na Waziri hadi jimboni kwake mkoani Mbeya kwa
barabara ya lami lakini kutoka Dodoma hadi Tabora ni kilomita kama 400 lakini
ukifika mgongo unauma kutoka na ubovu wa barabara,” alisema.
Akizungumzia usafiri wa anga, Dkt.
Kigwangalla alisema ni aibu kwa Tanzania kukosa ndege hata moja inayokwenda nje
ya nchi ambapo hali hiyo inatokana na uongozi mbovu si vinginevyo kwani Wachina
wakitumika vizuri wataleta maendeleo nchini.
Alisema China ni rafiki mzuri wa
Tanzania hivyo Serikali inaweza kuzungumza nao ipewe mkopo au kuzungumza na
kampuni kubwa zinazotengeneza ndege na kuingia nao mkataba ili kuwepo na safari
za nje ya nchi.
Hata
hivyo Bunge lilipitisha Bajeti ya Wizara hiyo zaidi ya sh. bilioni 491.
Masuala ya TRA kwa kweli yanaudhi! Kwa mfano ukihitaji huduma katika ofisi za TRA (Moshi) ukaenda mwenyewe, utazungushwa - njoo baadaye, njoo kesho, kesho kutwa....! Lakini ukiwatumia "vishoka" au waajiriwa WA WAFANYAKAZI WA TRA, ambao wako hapo nje tu kwa wingi (bila vitambulisho) mambo yako yatakuwa ni kufumba na kufumbua umepata risit au huduma unayoihitaji. Kama ndivyo kwanini serikali isihalalishe VISHOKA na kututangazia rasmi kwamba hatuwezi kupata huduma katika ofisi hizi (TRA) bila kupitia kwa VISHOKA???
ReplyDeleteNi kweli kabisa hili kuhusu VISHOKA! Hata mimi mwaka jana nilikuwa hapo moshi katika ofisi za TRA kulipia Road License ya gari yetu ya nyumbani! Nilitumwa kwenda benki, unga folen, lipia huko alafu ndo uje! Kwanza niliulizwa, "Nani kakutuma hapa?" Katika kushangaa na kuuliza "wanaujua mji" niliambiwa tumia KISHOKA! Baada ya kuongea na jamaa mmoja akaniambia nimpe Shs. 10,000/= na hizo karatasi zangu. Nikakaa hapo nje kusubiri na kabla sijamaliza coca cola moja nikaletewa risit za malipo na kila kitu kikiwa tayari! Nikaambiwa nirudi kesho kutwa yake kuchukuwa stika! Tukienda hivi, sisi Watanzania tutafika? TRA!TRA!TRA!TRA!TRA!TRA!TRA! sikilizeni kilio chetu!!
ReplyDelete