16 May 2013

Serikali yatangaza mikakati kupunguza umaskini nchini

Na David John


 IMEELEZWA kuwa katika kufikia Dira ya Maendeleo ya Taifa (VISION 2025) Tanzania imejiwekea mikakati mbalimbali ikiwemo MKUKUTA yenye malengo ya kuhakikisha kiwango cha ukosefu wa ajira kinapungua.
Akizungumza katika mkutano uliwakutanisha wadau mbalimbali wa maendeleo nchini Dar es Salaam jana Mkurugenzi Mkuu wa Ajira, Ally Msack alisema malengo hayo yanalenga kupunguza ajira isiyotimilifu, utumikishwaji wa watoto unapungua na uwepo wa hifadhi ya jamii kutokana na ajira.
Msack aliongeza kuwa kwa sasa imebakia miaka miwili kufikia malengo ya

maendeleo ya Millenia MDGS ambapo mwaka 2015, malengo ya Mkukuta11 2010/11 -2014/15 na malengo ya Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa miaka mitano 2011/12-2015/16 ambapo nchi inapaswa kutoa taarifa ya viwango vya viashiria vya malengo hayo.
Alisema kwa Tanzania zaidi ya asilimia 75.1 ya watu wenye uwezo wa kufanya kazi wanajihusisha na shughuli zilizopo katika sekta zisizo rasmi kwa maana hiyo utafiti unagusa sehemu kubwa ya nguvu kazi na utaiwezesha Serikali kupata picha halisi ya hali ya ajira nchini.
"Unajua utafiti huu unawezesha kutoa taarifa juu ya hali ya ajira nchini katika sekta rasmi na isiyo rasmi, utumikishwaji wa watoto, hali ya hifadhi ya jamii, hali kipato nchini, matumizi ya muda na ajira mpya zilizozalishwa katika sekta zote kwa kipindi husika (2006-2013).
Alisema viashiria hivi vya soko la ajira ndiyo kigezo kikubwa kinachotokea picha halisi ya mafanikio ya kiuchumi na kuchochea maendeleo ya nchi.
Aliongeza kuwa kwa mara ya mwisho utafiti huo ulifanyika mwaka 2006 na kuwezesha nchi kupata viashiria vyote muhimu vya soko la ajira vikiwemo vya MkukutaMalengo ya Maendeleo ya Millenia MDGS mipango ya maendeleo ya Taifa na kazi yenye staha.
Hata hivyo ili kupanga matumizi sahihi nguvu kazi kwa maendeleo ya kiuchumi lazima nchi iwe na taarifa sahihi ya soko la ajira, hivyo mchakato huo wa masuala ya ajira na kazi ni masuala mtambuka ambayo juhudi za pamoja zinahitajika kati ya Serikali na taasisi za elimu na utafiti wawekezaji, mashirika yasiyo ya kiserikali, wabia wa maendeleo waandishi wa habari na wananchi kwa ujumla ili kufikia malengo waliyojiwekea.

No comments:

Post a Comment