KAMATI ya Siasa
ya Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi na Sekretarieti ya halmashauri kuu ya
chama hicho Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imesema haijaridhishwa na
ujenzi wa daraja la Rau Mbokomu linalojengwa na Halmashauri ya Manispaa ya
Moshi, hivyo kuitaka manispaa hiyo kupitia upya ujenzi huo na kuhakikisha
magari makubwa hayapiti, hadi pale litakapothibitishwa kuwa liko imara.
Daraja hilo ambalo litagharimu sh.
milioni 102 bado halijakamilika lakini limeonekana kubomoka, hali ambayo
imesababisha watu kuhofia kuwa
hata kama litakamilika na kukabidhiwa linaweza
kuleta maafa kutokana na kujengwa chini ya kiwango.
Akizungumza wakati wa ukaguzi wa
miradi iliyotekelezwa na manispaa kwa kipindi cha mwaka 2012/2013 Katibu wa CCM
Manispaa ya Moshi, Aluu Segamba, alisema wao hawajaridhishwa na ujenzi wa
daraja hilo ambalo lina umuhimu mkubwa kwa wananchi.
"Sisi si wataalamu lakini naomba
niseme kuwa hatujaaridhishwa na ujenzi wa daraja hili,kwani haiwezekani daraja
lijengwe halijakamilika lakini libomoke, kunahitajika uangalizi mkubwa hapa ili
kuhakikisha daraja hili linakamilishwa kwa kiwango kinachostahili ili kuokoa
maafa yatakayoweza kutokea kutokana na kukamilisha chini ya kiwango," alisema
Segamba.
Aidha Segamba alisema kwa sasa wanaangalia
uwezekano wa kutuma wataalamu ili kwenda kukagua daraja hilo na kujiridhisha
kabla halijaanza kutumika.
Katibu huyo alishauri daraja hilo
lisitumike kupitisha magari makubwa hata baada ya kukabidhiwa hadi pale
watakapokwenda wataalamu kukagua na kujiridhisha hatua ambayo itasaidia kuepuka
maafa.
Mjumbe wa NecManispaa ya Moshi, Agrey
Marialle alisema licha ya taarifa kutolewa kuwa daraja hilo limeshakamilika kwa
asilimia 80 bado kazi ni kubwa na inahitaji umakini wa hali ya juu.
Kwa upande wake mkadiriaji wa ujenzi
manispaa hiyo, Charles Huka akizungumza kwa niaba ya mkandarasi wa manispaa
hiyo alisema wao wanaridhishwa na ujenzi wa daraja hilo ambalo limekamilika kwa
asilimia 80 na kwamba linatarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.
Kwa upande wake Eveta Lyimo msaidizi
wa mchumi wa manispaa hiyo alisema mradi wa daraja hilo ambao uliibuliwa na
wananchi kama mradi wa TASAF ulianza kujengwa mwaka 2009/2010 na kwamba
ulihitajika uwe umekamilika lakini kutokana na mvua umeshindwa kukamilika kwa
wakati uliopangwa.
No comments:
Post a Comment