18 March 2013

Waislamu Morogoro wampinga Mufti Simba

Na Aziz Msuya, Morogoro

SAKALA la Shekhe Mkuu wa Tanzania, Mufti Issa Bin Shaaban Simba, kumvua uongozi Shekhe Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Yahaya Samwali, sasa limeanza kuchukua sura mpya.

Hali hiyo inatokana na baadhi ya Waislamu mkoani humo, kupinga uamuzi wa Mufti Simba na kudai wamechoka kuburuzwa na Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA).

Akizungumza na waumini waliohudhuria swala ya adhuhuri iliyofanyika juzi katika Msikiti Mkuu wa Morogoro ulioko Mtaa
wa Boma, mmoja wa Wahadhiri wa Msikiti huo Ustaadhi Rashid Mlonge, alisema Waislamu mkoani humo hawawezi kuburuzwa
na chombo hicho kama miti au wanyama.

Alisema BAKWATA kupitia Baraza la Maulamaa, walimvua madaraka Shekhe Semwali kwa madai ya kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu mkoani humo jambo ambalo si kweli.

Ustadh Mlonge alisema, Waislamu mkoani humo wana akili timamu na hawako tayari kuburuzwa kama wafuasi wa chama cha siasa na hawapo tayari kumruhusu Shekhe Mustafa Shaaban kutoka mkoani Dodoma, kuhutubia chochote ndani ya msikiti huo.

Shekhe Shaaban aliteuliwa na Mufti Simba kukaimu nafasi ya Shekhe Semwali na kusimamia mchakato wa uchaguzi wa Shekhe Mkuu wa Mkoa ndani ya siku 90.

“Kama Shekhe Shaaban ambaye namfahamu vizuri atakuja
katika Msikiti huu, tutaswali sala mbili...BAWKATA hawawezi kutuburuza kama hatuna akili,” alisisitiza Ustaadhi Mlonge huku waumini wakipaza sauti na kusema takibiir.

Kumekua na mvutano mkali juu ya maamuzi yaliyofanywa na BAKWATA ya kumvua madaraka Shekhe wa Mkoa huo ambapo baadhi ya waumini wanapinga uamuzi huo na kudai chombo hicho kimekuwa kikifanya mambo yake kama chama cha siasa badala
ya mambo ya imani hivyo kutengeneza makundi ambayo
huchangia kudhoofisha maendeleo ya Waislamu.

Mwanzoni mwa Februari mwaka huu, Mufti Simba alimvua madaraka Shekhe Semwali kwa madai ya kushindwa kusimamia maendeleo ya Waislamu mkoani humo na kuagiza uchaguzi ufanyike ndani ya siku 90 ili kujaza nafasi hiyo uamuzi ambao umekua ukihojiwa na waumini mbalimbali.

“Huyu Shekhe Semwali hakuteuliwa na Mufti bali amechaguliwa
na Waislamu mkoani hapa sasa kwa nini aondolewe kienyeji, walioapaswa kulalamika kwa Mufti kwamba hatufai ni sisi tuliomchagua na hatujafanya hivyo vipi aondolewe,” alilalamika muumini mmoja aliyekuwa akitoka katika ibada hiyo.

Mwenyekiti wa Halmashauri ya BAKWATA mkoani humo, Bw. Fadhili Nyoni, aliwahi kunukuliwa na gazeti hili akisema kwamba, mchakato wa uchaguzi huo unakwenda vizuri.

Alisema wao kama halmashauri, kazi yao ni kutekeleza maelekezo kutoka ngazi za juu yanayotolewa na BAKWATA kupitia Baraza
la Maulamaaambapo kazi waliyonayo ni uhamasishaji ili watu wajitokeze kugombea nafasi hiyo.

2 comments:

  1. Hongereni kwa maamuzi mnayofikiria kuchukua bakwata hawako kwa maslahi ya waislamu bali kwa maslahi ya watu wachache. Wko tayari kufarakanisha,kusema uongo,kuchongea hata kuua kwa sababu ya DUNIA SIO KWA SABABU YA ALLAH.

    ReplyDelete
  2. Hongereni kwa maamuzi mnayofikiria kuchukua bakwata hawako kwa maslahi ya waislamu bali kwa maslahi ya watu wachache. Wko tayari kufarakanisha,kusema uongo,kuchongea hata kuua kwa sababu ya DUNIA SIO KWA SABABU YA ALLAH.

    ReplyDelete