11 March 2013

Polisi wakiri kuua raia kwa risasi


Na Damiano Mkumbo, Singida

MKAZI wa Bariadi, mkoani Simiyu, Methusala Shing'oma (36), amefariki dunia baada ya kupigwa risasi na polisi ambao walikuwa wakipambana na majambazi walioyateka magari mawili moja likiwa na maiti mbili pamoja na lori la mbao kwenye Kijiji Milade, Wilaya
ya Mkalama, Barabara ya Singida-Nzega.


Kamanda wa Polisi Mkoa mkoani Singida, Linus Sinzumwa, aliyasema hayo juzi wakati akitoa taarifa ya tukio hilo ambalo
lilitokea Machi 2 mwaka huu.

Alisema marehemu alifariki papo hapo baada ya polisi kufika
eneo la tukio na kuanza kufukuzana na majambazi walioyateka magari  na baada ya kumuona Shing'oma akiwa ameshika panga
mkononi walijihami wakidhani ni mmoja kati ya wahalifu hao.

“Baada ya kumchunguza marehemu, kumbe alikuwa dereva wa
lori aina ya Scania iliyokuwa na shehena ya mbao lenye namba
za usajili T 490 BTE na trela lake namba T 150 BFT, likitokea mkoani Iringa kwenda jijini Mwanza,” alisema.

Aliongeza kuwa, tukio hilo lilitokea saa saba usiku ambapo majambazi hao waliyateka magari mawili baada ya kuweka
mawe makubwa barabarani.

Kamanda Sinzumwa alisema, gari la kwanza kutekwa lilikuwa
Costa yenye namba za usajili T 968 CBN, ikitokea Dar es Salaam kwenda Tarime likiwa na miili ya marehemu wawili.

“Abiria waliokuwa kwenye gari iliyobeba miili pamoja na
roli ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva aliyepigwa risasi,
waliporwa vitu mbalimbali zikiwemo fedha taslimu na simu za
mikononi ambavyo thamani yake haijajulikana.

“Wakati majambazi hawa wakifanya upekuzi kwa abiria waliokuwa katika magari haya, polisi walifika eneo la tukio na kuanza kurusha risasi hewani hivyo kuleta hofu kwa majambazi ambao walianza kukimbia huku wakifukuzwa lakini walitokomea porini,” alisema.

Alisema mwili wa marehemu ulihifadhiwa katika chumba cha
maiti katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa huo kwa uchunguzi
zaidi ambapo jeshi hilo limeunda timu kuchunguza zaidi
mazingira ya tukio hilo.

Hata hivyo, alisema kuwa msako mkali unaendelea ili kuwanasa majambazi hao ambapo hadi jana, watu wanne walikamatwa
wakituhumiwa kuhusika na tukio la utekaji magari.

No comments:

Post a Comment