11 March 2013

Lipumba ataka wakazi wa Mtwara wasikilizwe


Na Said  Hauni, Lindi

CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeishauri Serikali kutopuuzia madai ya wakazi wa Mtwara kupinga usafirishaji wa gesi asilia
kwa njia ya bomba kutoka Kijiji cha Mnazi Bay, mkoani humo
na kuipeleka mikoa mingine ili kuzalisha umeme.

Ushauri huo umetolewa juzi na Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF) Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, wakati akiwahutubia wananchi katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Viwanja vya Shule ya Mpilipili, mkoani Lindi.

Mkutano huo ulihudhuriwa na wananchi kutoka Wilaya
mbalimbali za Mkoa huo na Mtwara ambapo Prof. Lipumba
alisema, gharama za kusafirisha umeme kwa njia za waya
ni nafuu zaidi ukilinganisha na usafirishaji gesi kwa bomba.

“Kauli zinazotolewa na viongozi mbalimbali wa Serikali waliopo madarakani akiwemo Rais Jakaya Kikwete, juu ya mpango wa kuisafirisha gesi, zinawafanya wananchi kukatishwa tamaa ya kunufaika na rasilimali hii katika maeneo yao.

“Naibu Waziri wa Nishati na Madini Stephen Masele, akiwa
mkoani Arusha kwenye mkutano wa wadau wa gesi mwaka
huu, alisema kusafirisha umeme kwa njia ya waya kupitia
nguzo ni gharama kubwa tofauti na kusafirisha gesi kwa
njia ya bomba bila kutoa mchanganuo,” alisema.

Prof. Lipumba alisema ilani ya uchaguzi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2010, Rais Kikwete wakati akiomba ridhaa ya kuchaguliwa katika nafasi ya urais, alisema taratibu zote
pamoja na ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji umeme wa
megaiti zaidi ya 300 kutokana na gesi hiyo utafanyika
ndani ya Mkoa huo.

“Gesi asilia iliyopo kisiwa cha Songosongo, katika Wilaya ya
Kilwa, Serikali iliahidi kujenga kiwanda cha mbolea (KILAMCO), kutokana na taka za gesi lakini hoja ya kuiondoa, imesababisha mpango wa ujenzi huo kusimama,” alisema.

Aliongeza kuwa, kutokana na hali hiyo, wananchi wa Mtwara na majirani zao (Mkoa wa Lindi), wamekosa imani na Serikali yao.

“Nchi ya Marekani iligundulika gesi katika moja ya majimbo
yake na haikuondolewa kupelekwa sehemu nyingine badala yake, walijenga kinu cha uzalishaji umeme katika eneo husika.

“Gharama za kusafirisha umeme wa msongo (nguzo) ni kubwa inayofikia dila za Marekani milioni 500, wakati usafirishaji gesi
kwa njia ya bomba gharama yake ni zaidi dola za Marekani
bilioni 1.3 kwa kilomita moja,” alisema Prof. Lipumba.

Alisema tayari Serikali imechukuwa fedha dola za Marekani
milioni 684 milioni kwa ajili ya ujenzi wa kiwanda cha uzalishaji
na gridi ya Taifa mkoani Mtwara, lakini anashangaa kuona mpango huo ukibadilisha badala yake wanataaka kusafirisha gesi.

Prof. Lipumba alifanya ziara ya siku moja mkoani Lindi na mikutano miwili ya hadhara mmoja ulifanyika asubuhi kwenye
Kata ya Mingoyo na mwingine jioni Mjini Lindi.

No comments:

Post a Comment