19 March 2013

NCCR-Mageuzi wamsamehe Kafulila


Na Mwajabu Kigaza, Kigoma

MBUGE wa Kigoma Kusini kwa tiketi ya Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. David Kafulila, amekiri kufanya kosa la utovu wa nidhamu ndani ya chama hicho na kusababisha uongozi kutaka kumvua uanachama.


Katibu Mkuu wa chama hicho, Samuel Ruhuza, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki katika mkutano wa hadhara uliofanyika katika katika Kata ya Nguruka Mkoani Kigoma ambao ulihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa chama hicho.

Alisema pamoja na Bw. Kafulila kukiri kosa na kuomba radhi, wananchi jimboni kwake na viongozi wa chama hicho walikiomba chama kimsamehe ili wasiweze kupoteza jimbo hilo.

“Hoja ya viongozi na wananchi ni kwamba, Bw. Kafulila bado ankipenda chama hiki ambacho ataendelea kukitumikia ili kutetea masilahi yao,” alisema Bw. Ruhuza na kuongeza kuwa, ugomvi uliokuwepo kati ya mbunge huyo na Mwenyekiti wa chama hicho Taifa, Bw. James Mbatia haupo tena.

Aliwataka wananchi na viongozi wote wa cham hicho jimboni humo kumpa ushirikiano Bw. Kafulila ili aweze kutetea masilahi yao kikamilifu.

“Mheshimiwa Kafulila alikaa, kutafakari na kugundua kuwa alichokuwa anakifanya si sahihi hivyo aliamua kuomba radhi
lakini kabla ya kusamehewa, alipewa mashariti ya kutimiza
vigezo ili msamaha wake uweze kukubaliwa, hadi sasa tayari ametimiza masharti yote kwa mujibu wa katiba na taratibu
za chama chetu,” alisema.

Alisema Halmashauri Kuu ya chama hicho, ilikaa kikao Septemba 9,2012 na kupokea ombi la msamaha wa Bw. Kafulila na ulikubali kumsamehe.

Aliongeza kuwa, lengo la chama hicho kutaka kumfukuza Bw. Kafulila halikuwa baya bali walitaka kujenga nidhamu ndani ya chama ambayo ilikuwepo toka miaka mingi.

No comments:

Post a Comment