19 March 2013

JK: Nataka hospitali ya wazazi Dar



Rachel Balama na Rehema Mohamed

RAIS Jakaya Kikwete, ameziagiza Halmashauri za Jiji la Dar es Salaam kujenga hospitali ya wazazi ya Mkoa ili kupunguza mrundikano wa wagonjwa katika baadhi ya hospitali.

Alisema haoni sababu ya wajawazito kurundikana katika baadhi ya hospitali wakati upo uwezekano wa kujenga hospitali hiyo ambayo itakuwa ikiwahudumia wajawazito pekee.

Rais Kikwete alitoa agizo hilo Dar es salaam jana wakati akizungumza na viongozi mbalimbali wa Serikali na Chama
Cha Mapinduzi (CCM), alipokuwa kwenye ziara ya kukagua
shughuli za maendeleo wilayani Ilala.

“Jengeni hospitali ya wazazi ya Mkoa ili kupunguza msongamano wa wagonjwa katika baadhi ya hospitali...madiwani katika vikao vyenu vya halmashauri mnajadili kuuza viwanja wakati wananchi wana matatizo katika sekta ya afya,” alisema Rais Kikwete.

Rais Kikwete aliwashukia madiwani hao baada ya Mkuu wa Mkoa huo, Bw. Meck Sadiki kusoma taarifa iliyohusu upungufu wa vifo vya wajawazito na ongezeko la vifo vya watoto chini ya miaka mitano.

Katika hatua nyingine, Rais Kikwete, alisema Serikali ipo tayari kutoa sh. bilioni 8.1 kwa ajili ya kununuaa vifaa mbalimbali baada ya kukamilika ujenzi wa Jengo la Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Mishipa ya Fahamu Muhimbili (MOI).

Alisema jengo hilo litasaidia kuokoa wagonjwa wengi kwenda kupatiwa matibabu nje ya nchi ili waweze kuyapata nchini.

Akitoa taarifa za mradi huo ujulikanao kama MOI (iii), Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini, Charles Mutalemwa, alisema jengo hilo linajengwa kwa fedha za mkopo kutoka Mfuko wa Taifa wa Bima
ya Afya (NHIF) ambapo utagharibu sh. bilioni 17.96.

Ujenzi wa jengo hilo ulizinduliwa na Rais Kikwete ambaye pia alizindua maabara ya kisasa ya Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) ambayo ujenzi wake umegharimu sh. bilioni 2.7.

Aaliitaka TFDA kuhakikisha inafanya uchunguzi wa kina kuhakikisha dawa bandia haziingii sokoni.

Wakati huo huo, Rais Kikwete alizindua Chuo cha Tehama (VETA), mjini Kipawa na kuhoji mkakati wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi pamoja na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kuhusu mradi wa ufundishaji teknolojia hiyo kwa wanafunzi wa sekondali.

Alishangazwa na ukimya wa uendelezwaji mradi huo na kusema kuwa, ungeweza kuondoa tatizo la upungufu wa walimu nchini.

“Serikali ilizungumza na kampuni mbalimbali za teknolojia duniani ili kuona zinasaidiaje kutekeleza mradi huu...Wizara Elimu na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknologia nielezeni mradi
huu umeishia wapi na mje na majibu ya kuufufua.

“Mradi huu ulikuwa unatupeleka katika kizazi cha dunia ya nne
na hauwezi kufa,” alisema Rais Kikwete.

Akizungumza na gazeti hili kuhusu mradi huo, Mkurugenzi wa Teknolojia kutoka Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Mhandisi Zaipuna Yohana, alikiri mradi huo kufifia na kudai kuwa, kwa sasa upo katika nzuri kwani umeshilikisha Wizara husika na
kuungwanishwa katika Mkongo wa Taifa.

Naye Mkurugenzi wa VETA nchini, Mhandisi Zebadia Moshi, aliioomba Serikali iwaongezee eneo linalomilikiwa Serikali ya
Mtaa wa Kipawa lilolopo nyuma ya jengo la chuo hicho
ili waweze kukipanua.

No comments:

Post a Comment