18 March 2013

Mbunge afichua siri kutojiunga na JKT


Na Benedict Kaguo

MBUNGE wa Kisesa, mkoani Simiyu, Bw. Luhaga Mpina, ametoboa siri ya kukataa kujiunga na mafunzo ya Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), kutokana na wananchi wa jimbo hilo kukubwa na baa la njaa hali iliyowalazimu wengine kuzikimbia familia zao.

Bw. Mpina ambaye ni miongoni mwa wabunge vijana ambaye alitakiwa kujiunga na mafunzo hayo Machi mosi mwaka huu, alisema kutokana na hali hiyo alilazimika kuhamia kwenye
Ofisi ya Waziri Mkuu Kitengo cha Maafa ili kufuatilia
chakula cha msada hivyo kukosa muda na kujiunga.

Akizungumza na wananchi wa jimbo hilo juzi, Bw. Mpina
alisema alisema alishindwa kwenda kujiunga na mafunzo hayo
ili aweze kuwatumikia wananchi kwa tatizo walilonazo.

Alisema mafunzo ya JKT ni muhimu lakini kutokana na mazingira yaliyokuwepo kwa baadhi ya wananchi wa jimbo hilo kula mlo mmoja, alilazimika kufanya kazi ya ziada ili kuokoa maisha yao.

“Nawaomba msisononeke kwani Serikali inawathamini ila baadhi maofisa waliotumwa kuja kufanya tathmini juu ya hali ya chakula katika Wilaya ya Meatu hususani jimbo la Kisesa, waliishia katika mnada wa Malwilo na kukuta mahindi yakiuzwa na kuamini
Wilaya hii ina chakula cha kutosha,” alisema.

Bw. Mpina alisema, Serikali imekubali kuipatia Wilaya hiyo tani zaidi ya 2,500 za mahindi ambayo yatachukuliwa kutoka katika maghala ya chakula yaliyopo Dodoma na Shinyanga ili kuwapunguzia wananchi tatizo la njaa.

Wananchi hao, walimpongeza Bw. Mpina kwa kutoshiriki mafunzo hayo ili aweze kushughulikia tatizo la njaa jimboni kwake.

Walisema kwa sasa debe moja la mahindi linauzwa sh. 14,000 kutoka sh. 6,000 mwaka 2012, wakati bei ya ngombe imeshuka
kuutoka sh. 180,000 hadi sh 80,000, hivyo wanalazimika kununua
mahindi katika kipimo cha bakuli kinachouzwa sh. 1,500.

Walimtaka Bw. Mpina kuishinikiza Serikali idhibiti kushuka
kwa bei ya zao la pamba na kupanda bei ya vyakula kiholele
ili waweze kumudu gharama za maisha.

2 comments:

  1. wabunge waliokwenda JKT ni ubishoo tu,watu hawa tunawategemea muda si mrefu wawe bungeni kujadili bajeti ya serikali sasa ni lini watachukuwa mawazo na kero za wananchi ili wazipeleke bungeni?

    ReplyDelete
  2. Viongozi wetu,wasaidieni wananchi kupata mbinu bora za kulima na kuhifadhi mazao kwa matumizi ya baadae.Msisubiri njaa itokee ndo msimamie chakula cha msaada, huo si utatuzi wa kufaa kwa tatizo kama hilo.

    ReplyDelete