18 March 2013
Katibu Uenezi CCM Shy avuliwa uongozi
Na Suleiman Abeid, Shinyanga
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), Wilaya ya Shinyanga Mjini, kimemuondoa katika nafasi ya uongozi Katibu wake wa Itikadi, Siasa na Uenezi, Bw. Charles Shigino ikiwa ni miezi michache tangu achaguliwe katika wadhifa huo.
Taarifa zilizopatikana mjini hapa kutoka kwa baadhi ya wajumbe
wa Halmashauri Kuu ya CCM wilayani humo, zimesema uamuzi huo umefikiwa juzi baada ya kumalizika kikao cha Halmashauri
katika Wilaya hiyo.
Mmoja wa wajumbe hao ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini, alisema miongoni mwa tuhuma zilizokuwa zikimkabili
Bw. Shigino ni kuungana na wafanyabiashara ndogondogo (machinga) waliokuwa wakifanya biashara eneo la Shule ya
Msingi Town, kupinga kuondolewa katika eneo hilo bila kuwapatia eneo mbadala la kuendeshea biashara zao.
Jeshi la Polisi mjini humo lililazimika kutumia nguvu kubwa ili kuwaondoa wafanyabiashara huo katika eneo hilo.
“Kwa kipindi kirefu, Bw. Shigino amekuwa akilalamikiwa na viongozi wenzake kutokana na kitendo chake cha kwenda
kukutana na wananchi katika maeneo mbalimbali ili kumfikishia kero zao zinazosababishwa na uongozi wa Manispaa.
“Kero hizo ni pamoja na suala la miradi inayofadhiliwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) kutekelezwa chini ya kiwango kinachotakiwa,” alisema mjumbe huyo.
Alisema baadhi ya malalamiko yaliyofikishwa mbele ya kikao cha kamati hiyo dhidi ya Bw. Shigino ni kitendo chake cha kukemea ubadhirifu wa fedha sh. milioni 37 zilizotolewa na TASAF kwa ajili ya ujenzi wa lambo la kunyweshea mifugo kwenye Kata ya Ndembezi na ujenzi wa choo katika mnada wa Old Shinyanga.
Kutokana na hali hiyo, baadhi ya watendaji ndani ya manispaa hiyo akiwemo Diwani wa Kata ya Old Shinyanga, Frednand Kanukule walilalamikia kitendo cha Bw. Shigino kwenda moja kwa moja kukutana na wananchi.
Malalamiko ya wakazi wa Ndembezi waliyomweleza Bw. Shigino ni pamoja na tatizo la ujenzi wa lambo la kunyweshea mifugo ambalo mbali ya kutumia fedha nyingi halijakamilika na limechimbwa mfano wa jaruba la kupandia mpunga.
Sakata la choo katika eneo la Mnada wa Old Shinyanga kinachodaiwa kujengwa kwa gharama za sh. milioni 15 zilizotolewa na manispaa hiyo, wanachama wa CCM, Kata ya Old Shinyanga walipinga ujenzi huo wakidai umefanyika chini ya kiwango.
Katika mkutano wa hadhara uliokuwa umeitishwa na wana CCM
wa kata hiyo na kumkaribisha Bw. Shigino, wanachama hao waliwakataa baadhi ya viongozi wao akiwemo diwani wa kata hiyo na Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Old Shinyanga kwa madai ya kushindwa kusimamia miradi ya maendeleo katika kata yao.
Akizungumza na gazeti hili jana, Bw. Shigino alikiri kupokea
taarifa za kuondolewa katika wadhifa huo na kudai kuwa, asingeweza kuzungumzia kirefu suala hilo kwanie hajakabidhiwa barua rasmi ya maamuzi hayo na kuongeza kuwa, sababu kubwa ni kitendo chake cha kuwatetea wananchi.
Kwa upande wake, Katibu wa CCM Shinyanga Mjini, Mberito Magova alikiri Bw. Shigino kuondolewa katika uongozi na kudai kuwa, uthibitisho wa maamuzi yao utatolewa na vikao vya juu
baada ya kupitia maelezo yaliyopelekwa kwao.
“Ni kweli Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya juzi iliamua kumuondoa katika wadhifa wake kutokana na tuhuma mbalimbali anazotuhumiwa, sisi sio wa mwisho kufikia maamuzi, tumepeleka mbele mapendekezo yetu yakikubaliwa yatatekelezwa kwa sasa siwezi kusema mengi,” alieleza Magova.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment