12 March 2013

Mbatia amtaka Raila Odinga kuheshimu matokeo



Na David John

MWENYEKITI wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Bw. James
Mbatia, amemshauri aliyekuwa mgombea urais nchini Kenya
kwa tiketi ya Chama cha Muungano CORD, Bw. Raila Odinga kuheshimu matokeo ambayo ndio maamuzi ya wananchi.

Alisema kinachohitajika baada ya Bw. Uhuru Kenyatta kushinda nafasi ya urais nchini humo kwa tiketi ya Chama cha Muungano
wa Jubilee ni kukaa mezani ili kuijenga nchi hiyo kwa pamoja.

Akizungumza na waandishi wa habari Dar es salaam jana, Bw.
Mbatia alimpongeza Bw. Kenyatta kwa ushindi alioupata na
kusisitiza kuwa, Wakenya wamefanya uamuzi mgumu ambao haukutarajiwa na watu wengi.

“Hali nii inatokana na ukweli kwamba, Bw. Kenyatta anakabiliwa
na kesi mahakamani lakini bado wananchi wameendelea kumuamini na kumpa nchi ili aweze kuwaongoza kama rais wao.

“Ni vyema Bw. Odinga akaachana na nia yake ya kutaka kwenda mahakamani kuweka pingamizi la matokeo yaliyotangazwa badala yake aheshimu maamuzi ya Wakenya ambayo wameyafanya kwa kumchagua Bw. Kenyatta,” alisema.

Alisema Wakenya wameandika historia mpya duniani hasa katika Bara la Afrika inayopaswa kuigwa na mataifa mengine na kufafanua kuwa, kama Bw. Odinga atakwenda mahakamani kuweka pingamizi ajue wazi huko ni kutaka kuwagawa Wakenya, kuhatarisha amani ambayo tayari wameionyesha, kusababisha machafuko na chuki.

Bw. Mbatia aliongeza kuwa, ushindi wa Bw. Kenyatta ni kielelezo kuwa si kila kitu watakacho wazungu, waafrika wakifanye lakini ufike wakatiAfrika iweze kufanya maamuzi yake wenyewe bila kuingiliwa na taifa lolote duniani.

“Namuomba Bw. Odinga na wagombea wengine walioshindwa katika uchaguzi huu waheshimu makubaliano ya kulinda amani ambayo walikubaliana ili kuivusha Kenya kwenye demokrasia
ya ukomavu,” alisema Bw. Mbatia.

Katika hatua nyingi, Bw. Mbatia alizungumzia mchakato wa Katiba Mpya unaondelea nchini na kusisitiza nchi inapaswa kujifunza kwa yale mazuri ambayo Wakenya wameweza kuyatumia katika Katiba yao ambayo wameipata miaka michache iliyopita.

1 comment: