12 March 2013

Mtikila ampongeza Dkt .Nchimbi

Na Kassim Mahege

SIKU moja baada ya Waziri wa Mambo ya ndani Dkt.Emmanuel Nchimbi kuwasimamisha kazi maofisa wa Jeshi la Polisi kwa tuhuma mbalimbali, Mwenyekiti wa Chama Cha Democratic Party(DP) Mchungaji Christopha Mtikila amempongeza kwa hatua hiyo na kumtaka asiishie hapo.

Akizungumza na gazeti hili jana alisema kuwa hatua hiyo inaonyesha ishara nzuri kwa Jeshi la polisi lakini Dkt Nchimbi anatakiwa achimbuwe mizizi ya uhalifu kwa jeshi hilo na hatua kali za kisheria zichukuliwe kwa watakaobainika.

"Kuwasimamisha kazi pekeyake haitoshi tunataka ukweli ukibainika kwa maofisa hao hatua kali sana za kisheria zifanyike dhidi yao,maana hao ndio wanaolipaka matope Jeshi la Polisi."na kuongeza kuwa hao ndio wanaowaumiza wananchi."alisema Mtikila.

Akitolea mfano wa aliyekuwa waziri wa fedha Basil Mramba,Amatus Liyumba na Yona wa benki kuu mahakama yenyewe ilithibitisha kuwa hakuna makosa yoyote ya wizi walioyafanya ispokuwa makosa yao yalikuwa ni kutumia vibaya madaraka yao na kuongeza kuwa  leo hii watu hao wanasota kisutu,hivyo anataka na maofisa hao pia wapelekwe mahakamani ili iwe fundisho kwa wengine.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Dkt.Wilbroad Slaa alisema haoni kama kuna jipya kutokana na hatua hiyo.

"Mimi sitaki kuzungumzia uamuzi huo wa Dkt.Nchimbi kwa sababu ni dhahiri kuwa kuna double standard,Nchimbi aliwahi kuunda tume kwa ajili ya kufuatilia mauaji ya Mwangosi lakini hakuna hatua yoyote alioichukua mimi sioni kama kuna jambo jipya."alisema Slaa.

Alisema hatua hiyo imechelewa kutokana na kukithiri kwa vitendo vya uhalifu kwa jeshi la polisi na kutolea mfano kuwa Dkt.Nchimbi aliwahi kuunda tume yake kwa ajili ya kuchunguza mauaji ya mwangosi,Ripoti zote zilizotolewa zilionyesha kuwa Jeshi la polisi lilitumia nguvu isio ya lazima na kuongeza kuwa mpaka hivi leo Nchimbi hajasema chochote.

No comments:

Post a Comment