13 March 2013

MATOKEO IV Walimu waliopengezana kuchunguzwa *TCRA kusaka ujumbe waliotumiana katika simu zao



Na Rose Itono

SERIKALI itashirikiana na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), ili kuwabaini walimu waliopongezana kutokana na matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012.


Walimu hao wanadaiwa kushabikia matokeo hayo na kutumiana ujumbe mfupi wa maneno katika simu zao (sms), wakionesha kufurahishwa hali hiyo na kuitaka jamii kusubiri matokeo yajayo.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Mtandi Bunyanzu alisema ni aibu kwa walimu hao kupongezana kwa matokeo mabaya ya kidato cha nne mwaka 2012 wakati jamii ikitafuta suluhisho la tatizo hilo.

Alisema kutokana na hatua hiyo, Serikali itashirikiana na TCRA ili kuwabaini walimu hao ili waweze kuchukuliwa hatu za kisheria na kuhoji iweje mwalimu afurahie matokeo mabaya ya mwanafunzi wake wakati yeye ndiye anayewaandaa.

“Kinachofanywa na walimu hawa ni aibu kubwa kwa Taifa kwa sababu wao ndio wanaowaandaa...mchakato wa kuwabaini unaweza kuwa mgumu lakini Serikali itafanya kila jitihada kwa kushirikiana na TCRA ili kuwabaini,” alisema Bunyanzu.

Aliongeza kuwa, hivi karibuni umeibuka utaratibu kwa baadhi ya watu kutumia laini za simu ambazo hazijasajiliwa kwa kufanya maovu hivyo hivyo kama walimu hao watakuwa wamesajili namba zao, mchakato wa kuwakamata utakuwa rahisi.

Inadaiwa walimu hao mbali ya kupongezana pia walitumiana ujumbe unaosema “ukibishana na mpishi jiandae kula chakula kibichi, matokeo ya darasa la saba, kidato cha pili na nne
yanatokana na mpishi kusemwa vibaya eti hajui kupika.

Ujumbe huu uliongeza kuwa, matokeo mabaya mwaka 2012
ni hatua ya mwanzo na mwakani yatakuwa mabaya zaidi.

1 comment:

  1. martin nimeipenda hiyo tafuteni wapishi wapya kama vipi wachapwe viboko

    ReplyDelete