05 March 2013

Issa Ponda ana kesi ya kujibu *Mahakama yathibitisha mashtaka dhidi yao *Sasa kuanza kujitetea kuanzia Jumatano


Na Rehema Mohamed

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, imewaona Katibu wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu nchini, Shekhe Issa Ponda na wenzake 49, wana kesi ya kujibu.


Shekhe Ponda na wenzake, wanakabiliwa na kesi ya uchochezi
pamoja na wizi wa mali zenye thamani ya zaidi ya sh. milioni 59
ambapo washtakiwa wote watatakiwa kujitetea kuanzia Machi 6 mwaka huu.

Hakimu anayeisikiliza kesi hiyo, Bi. Victoria Nongwa, alitoa
uamuzi wa mahakama na kudai washtakiwa hao wana kesi ya
kujibu ambapo upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha
kesi yao na hivyo ni vyema washtakiwa wote wajitetee.

Alisema baadhi ya maelezo ya washtakiwa ambayo yaliwasilishwa mahakamani hapo, yanaonesha baadhi ya Waislamu hawajaridhishwa na kitendo cha Baraza la Waislamu nchini (BAKWATA), kubadilishana kiwanja namba 311/3/4/ Block T Chang'ombe Markaz na Kampuni ya Agritaza Ltd.

Hata hivyo, alisema mahakama haijazuia mtu yeyote kupinga uwamuzi wa BAKWATA katika mahakama zinazosimamia
migogoro ya ardhi.

Aliongeza kuwa, mahakama hiyo inaona ni vyema upande wa utetezi utoe utetezi wao kwa washtakiwa wote ili waseme walichokuwa wakikitafuta katika kiwanja hicho.

Hakimu Nongwa alisema ni wazi kwamba, mahakama hiyo
haiwezi kutatua migogoro ya ardhi lakini kutokana na ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo, inaonesha aliyepewa ardhi
hiyo ameweza kufanya mabadilishano kwa ekari 40 zilizopo Kisarawe, mkoani Pwani.

Baada ya kusoma uamuzi huo, Hakimu Nongwa alimtaka
wakili wa utetezi Bw. Juma Nassoro, kuileleza Mahakama
hiyo njia watakayotumia wateja wake kujitetea katika siku
ya kuanza kusikilizwa utetezi.

Februari 27 mwaka huu, mawakili wa pande zote katika kesi hiyo waliwasilisha hoja zao za kuona kama washtakiwa hao wana kesi
ya kujibu au la.

Wakati akiwasilisha hoja zake, Bw. Nassoro, aliiomba mahakama hiyo kuona washtakiwa wa kesi hiyo hawana kesi ya kujibu na
kutoa sababu mbalimbali.

Akitoa sababu hizo kwa kuainisha mashtaka yanayowakabili washtakiwa hao, Bw. Nassoro alidai katika shtaka la kula njama linalowakabili washtakiwa wote 50 na uchochezi linalomkabili Shekhe Ponda na Salehe Mkadam, alidai mahakama haitatenda
haki ikitaka washtakiwa hao wajitete kwa makosa hayo
kwani yaliandikwa kimakosa.

Alidai katika kosa la kula njama, hati ya mashtaka haikueleza washtakiwa hao walikula njama ya kutenda kosa gani ambapo
katika kosa la uchochezi, hati ya mashtaka pia haikueleza kama waliwashawi wafuasii wao kutenda kosa gani la jinai.

Katika kosa la kuingia kwa nguvu kijinai, Bw. Nassoro alidai
kosa hilo lisingekuwepo kwa sababu mazingira ya kesi hiyo yanaonesha kuna mgogoro wa umiliki wa ardhi.

Alidai kisheria mahakama hiyo haiwezi kutoa uwamuzi kwa
kosa la kuingia kwa nguvu kijinai bila kuamua mgogoro wa umilikaji wa ardi uliopo.

Aliongeza kuwa, upande wa mashtaka ulishindwa kupeleka vielelezo vya anayedai mmiliki halali wa eneo hilo ikiwemo
hati badala yake wamepeleka barua kutoa ofisi ya ardhi.

Katika kosa la wizi, Bw. Nassoro alidai kosa hilo halikuletewa ushahidi wa kutosha ambapo upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kama vifaa vya ujenzi vinavyodaiwa kuibwa
vilikuwepo eneo la tukio.

Alisema ushahidi uliowasilishwa mahakamani hapo na upande wa mashtaka, haujaweza kuthibitisha makosa dhidi ya washtakiwa pasipo kuacha shaka na kusababisha washtakiwa hao wajitetee.

Kwa upande wake, wakili wa Serikali Bw. Tumaini Kweka, akijibu hoja hizo, aliiomba mahakama kuwaona washtakiwa wote wana kesi ya kujibu kwa sababu upande wa mashtaka umeweza kuthibitisha mashtaka dhidi yao.

*Mahakama yathibitisha mashtaka dhidi yao
*


Katika kesi hiyo, upande wa mashtaka ulikuwa na mashahidi 17 miongoni mwao wakitoka BAKWATA, wajumbe wa Baraza la Maulamaa, wapelelezi wa kesi hiyo na anayedaiwa kuwa mmiliki wa eneo lililovamiwa na washtakiwa la Agritaza Ltd.

Shekhe Ponda na wenzake wanakabiliwa na makosa matato ambapo Oktoba 12 ,2012 wanadaiwa kula njama na kuvamia kiwanja kinachomilikiwa na kampuni hiyo ili kujimilikisha isivyo halali.

No comments:

Post a Comment