26 February 2013

'Waandishi wapatiwe mafunzo ya usalama'Na Anna Titus

MRATIBU wa Kitaifa wa Mtandao Unaotetea Haki za Binadamu nchini, Bw. Onesmo Olengurumwa, amezitaka taasisi za vyombo vya habari, kutoa mafunzo ya usalama kwa waandishi wa habari.


Mafunzo hayo yatasaidia kuimarisha usalma wa waandishi hasa katika matukio mbalimbali ya vurugu kutokana na vitendo vya ukatili vinavyoendelea dhidi yao wawapo kazini.

Bw. Olengurumwa aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kusisitiza kuwa, hali ya kiusalama kwa mwandishi wa Kituo cha Televisheni cha ITV, mkoani Mwanza, Bw. Cosmas Makongo si nzuri.

Alisema Bw, Makongo mbali ya kufanya kazi yenye masilahi kwa jamii na Taifa kwa ujumla, amekuwa akipokea simu za vitisho kutoka kwa watu mbalimbali na kumtishia usalama wake.

Aliongeza kuwa, baadhi ya ujumbe mfupi anaotumiwa katika simu yake ya mkononi (sms), una maneno yanayosema “umetufuatilia kwa muda mrefu, sasa umefika mwisho wako” ambapo ujumbe mwingine ulisomeka kuwa, “Makongo wewe ni kikwazo cha
watu wengi, tutahakikisha tunakushughulikia”.


Alisema kwa hali hiyo ni wazi kuwa Bw. Makongo ambaye ni mtetezi wa haki za binadamu hayupo salama kwani haifahamiki
ni lini maadui zake wanaweza kutekeleza azma yao.

“Mtandao wetu utahakikisha unafuatilia kwa karibu suala hili ili kujua hatima yake pamoja na ukatili wanaofanyiwa waandishi wa habari waliotaka kufanyiwa mkoani Mtwara,” alisema.

Bw. Olengurumwa aliongeza kuwa, mtandao huo haujaridhishwa
na utendaji kazi wa Jeshi la Polisi nchini kutokana na kifo cha mtetezi wa haki za binadamu ambaye alikuwa Mkurugenzi wa Mtendaji wa Shirika la Action Based Foundation (ABC), EustaceNyarugenda ambacho kina utata mkubwa.

Aliishauri Serikali iandae mazingira bora ya kazi kwa watetezi hao ili waweze kufanya kazi bila vitisho na kulitaka jeshi hilo mkoani Mara kufuatilia kwa undani kifo cha marehemu Nyarugenda.

1 comment:

  1. Binafsi sina imani sana na waandishi wa habari nahisi wapo wengine wanatumiwa na makundi yasiyo na nia njema na maisha ya watu au ni wabinafsi. Mfano tunasikia wanatutangazia mauaji ya walemavu wa ngozi na wale wanaoshikwa na viungo vya binadamu kwa madai ya biashara LAKINI sijawahi kuwasikia wamemtangaza aliewatuma wauaji kutekeleza unyama huo hata siku moja.

    ReplyDelete