26 February 2013

Shekhe 'atoboa' siri ya vurugu, mauaji, nchini


Na Heri Shaaban

MWENYEKITI wa Taasisi ya Kiislamu ya Imamu Bukhary, Shekhe Khalifa Khamis, amesema vurugu na mauaji yanayoendelea nchini yanachangiwa na udhaifu wa vyombo vya dola kutosimamia sheria zilizopo ili kukomesha vitendo hivyo kwenye jamii.

Hali hiyo imechangia mauaji ya viongozi wa dini bila sababu
za msingi, uharibifu wa mali pamoja na uchomaji makanisa.

Shekhe Khamis aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akizungumza na waandishi wa habari ili kulaani mauaji
yanayofanywa kwa viongozi wa dini.

“Mwaka 2012, kiongozi wa dini ya Kiislamu alimwagiwa tindikali Zanzibar...hadi leo wananchi hawajaelezwa hatua zilizochukuliwa
na hivi karibuni, yametokea mauaji ya Padri Evaristus Mushi, wananchi wametega masikio wakisubiri dola itafanya nini.

Aliiomba Serikali itoe taarifa kwa umma juu ya uchunguzi wa
matukio hayo ili wananchi waendelee kuiamini ambapo vitendo
vinavyofanywa na waumini wa Kiislamu kila siku za Ijumaa
vinatoa ujumbe kuwa, wakati umefika wa vyombo vya dola
kuchukua hatua za kuinusuru nchi isiingie katika machafuko.

“Inaonesha kipo kikundi cha watu wachache ambao wamechoka kuishi kwa amani, nawaomba Waislamu tuendelee kuilinda amani yetu na kutoa ushirikiano kwa vyombo vya dola ili wahusika wa vurugu na mauaji waweze kukamatwa,” alisema.

Shekhe Khamis alilaani kitendo cha Jumuiya ya Taasisi za Kiislamu nchini kusambaza vipeperushi vinavyoeneza chuki kati ya Wakristo, Waislamu, Serikali na kusababisha uvunjifu wa amani kila Ijumaa hasa kiongozi wao Shekhe Ponda Issa Ponda anapofikishwa mahakamani.

“Uislamu haufundishi kujichukulia sheria mikononi, kupuuza na kutoheshimu mamlaka ya dola, vyombo vya sheria, kujitumbukiza katika maandamano ya kushinikiza Serikali au mahakama kumwachia kiongozi wa dini,” alisema.

No comments:

Post a Comment