26 February 2013

'Serikali iyafanyie kazi madai ya walimu'


Na Yusuph Mussa, Lushoto

SERIKALI imeshauriwa kuyafanyia kazi madai mbalimbali ya walimu nchini kwani matokeo mabaya ya wanafunzi wa kidato
cha nne, yamechangiwa na madai yao kutofanyiwa kazi.

Mkuu wa Shule ya Sekondari ya Wasichana ya St. Mary's Mazinde Juu, iliyopo Kata ya Magamba, Wilaya ya Lushoto, mkoani Tanga, Mtawa Evetha Kilamba, aliyasema hayo mwishoni mwa wiki  kwenye mahafali ya 16 ya kidato cha sita shuleni hapo.

“Tunaiomba Serikali ijali na kusikiliza matakwa ya walimu, wasiposikilizwa madhara yake ni makubwa na mfano halisi
ni matokeo ya kidato cha pili na kidato cha nne mwaka 2012.

“Matokeo yanasikitisha, upo umuhimu wa kuziboresha shule za
kata ili ziweze kufanya vizuri kwa faida ya Watanzania wote,
kwani pamoja na shule yetu kushika nafasi ya nane kitaifa,
bado tunazisikitikia shule za kata,” alisema.

Alisema shule hiyo ipo tayari kushirikiana na shule jirani za kata ili kuinua kiwango cha elimu kwa shule hizo kwani lengo lao ni kuona kila mtoto mtoto wa Kitanzania anapata elimu bora si bora elimu,” alisema Mtawa Kilamba.

Aliongeza kuwa, mafanikio waliyopata yametokana na ushirikiano uliopo kati ya uongozi wa shule,bodi yao, wazazi na wanafunzi kujituma zaidi kwenye masomo.

Mwenyekiti wa Bodi ya shule hiyo, ambaye pia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa mkoani Arusha (AICC), Elishilia Kaaya, alisema shule hiyo imefanikiwa
kudhibiti nidhamu kwa wanafunzi na matumizi ya simu.

“Baada ya kuhitimu masomo yenu, hivi sasa mnakwenda mtaani hivyo mnapaswa kuzingatia yale mliyofundishwa, nitashangaa kama mtaanza kuitwa majina ya ajabu kwa sababu ya kukosa maadili,” alisema.

No comments:

Post a Comment