18 February 2013

Pinda awaonya Maofisa wa PolisiNa Pendo Mtibuche, Dodoma

SERIKALI imesema kuwa, viongozi wa Jeshi la Polisi nchini
ambao watabainika kutoa amri kwa askari walio chini yao na kusababisha wavunje sheria, watachukuliwa hatua.


Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, aliyasema hayo mjini Dodoma juzi wakati akifunga Mkutano Mkuu wa Jeshi la Polisi uliofanyika kwa siku nne ukishirikisha Maofisa wa jeshi hilo.

Alisema kwa kuzingatia nidhamu ya jeshi hilo, askari hupokea
amri, maelekezo kutoka kwa viongozi wao ambayo baadhi yake yanakinzana na sheria za nchi.

“Ili tuweze kutenda haki na kuimarisha uwajibikaji, lazima hatua stahiki zichukuliwe kwa viongozi wa jeshi ambao watabainika
kutoa amri, maelekezo yatakayosababisha askari kuvunja sheria.

“Hapa lazima mfahamu kwamba, mhalifu hajapewa nguvu kisheria na ndiyo maana havunji haki za binadamu isipokuwa anatenda kosa la jinai hivyo askari anayempiga mtuhumiwa wakati wa mahojiano, atakuwa emetenda kosa la jinai la shambulio.

“Pia atakuwa amevunja sheria ya haki za binadamu zinazotaka vyombo vya dola kutowatesa watuhumiwa,” alisema Bw. Pinda
na kuongeza kuwa, kutokana na hali hiyo Serikali imekuwa ikiunda tume za uchunguzi dhidi ya vitendo vinavyofanywa na baadhi ya

askari wanaobainika kutenda makosa ya jinai na yale
yanayokiuka haki za binadamu.

Alisema si nia ya Serikali kujichunguza yenyewe lakini jamii inapolalamika kwa kukosa majibu sahihi kutoka ndani ya jeshi
hilo juu ya haki iliyovunjwa, lazima Serikali iwajibike kwa wananachi wake kuunda tume huru ya uchunguzi ili
kubaini ukweli na kuwezesha haki itendeke.

Aliongeza kuwa, wakati wote tume hizo zinapoundwa, kumekuwa na gharama kubwa kwa Serikali na kuhoji Serikali itaendelea kuunda tume za kulichunguza jeshi hilo hadi lini?

“Nataka kuwaeleza wazi kuwa, majibu yanayotolewa na Jeshi la Polisi, inapobainika kuna ukweli uliopotoshwa kuhusu tukio fulani wananchi hukosa imani na Serikali yao pamoja na jeshi letu,” alisema.

Akizungumzia suala la rushwa, Bw. Pinda alisema suala hilo ni miongoni mwa eneo ambalo lipo ndani ya jeshi hilo hususan katika Kikosi cha Usalma Barabarani ambacho kimekuwa kikilalamikiwa
sana na madereva wa ngazi zote kuanzia wa daladala, mabasi makubwa, malori na magari binafsi.

No comments:

Post a Comment