18 February 2013

Mnyika kuongoza maandamano ya kudai maji Dar


Na Stella Aron

MBUNGE wa Jimbo la Ubungo, Bw. John Mnyika (CHADEMA), anatarajia kuongoza maandamano ya wananchi kwenda Wizara ya Maji kama Waziri mwenye dhamana Profesa Jumanne Maghembe, atashindwa kutoa majibu kwa umma juu ya utatuzi wa kero ya
maji jijini Dar es Salaam.


Taarifa aliyoitoa kwa vyombo vya habari Dar es Salaam jana, Bw. Mnyika alisema Februari 10 mwaka huu, aliliwasilisha suala hilo
kwa wananchi na kutoa wiki mbili kwa Prof. Maghembe kujitokeza kwa umma ili kutoa majibu aliyokwepa kuyatoa bungeni, Dodoma.

Alisema katika taarifa, alieleza wazi kuwa kama Prof. Maghembe atashindwa kuzungumzia tatizo hilo, ataongoza maandamano kwenda wizarani ili kushinikiza Serikali ichukua hatua.

Aliongeza kuwa, kwa nyakati tofauti kuanzia Januari hadi Februari mwaka huu, limetokea tatizo la kuharibika baadhi ya mitambo inayotumika kuzalisha maji katika vyanzo vya Mto Ruvu hivyo kusababisha tatizo la maji kwa wakazi wa Dar es Salaam.

“Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA), imeingia mkataba wa uendeshaji na Kampuni ya Maji Safi na Maji Taka Dar es Salaam (DAWASCO), wa kutekeleza majukumu mbalimbali ikiwemo kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji wa maji, kufanya matengenezo na kutoa taarifa kwa wananchi kuhusu huduma zinazotolewa.

“Kinachoendelea sasa, DAWASA na DAWASCO wameshindwa kufanya matengenezo ya mitambo kwa wakati ili kukabiliana na upungufu wa uzalishaji maji Dar es Salaam hivyo Bunge lilipaswa kujadili hoja binafsi niliyoiwasilisha,” alisema.

Alisema kwa kuzingatia mikataba hiyo, DAWASA na DAWASCO wanapaswa kutoa matangazo kuhusu matatizo mapya yaliyojitokeza ili kuepusha matatizo yaliyopo kuhusishwa na hatua ya Bunge kuondoa hoja yake aliyoiwasilisha bungeni.

Bw. Mnyika aliongeza kuwa, mwaka 2005, DAWASA iliingia mkataba wa miaka 10 wa uendeshaji na DAWASCO ambayo ilipaswa kuendesha mitambo, kusimamia usambazaji maji, uondoshaji maji taka, kuuza maji na kutoa ankara kwa wateja, kukusanya maduhuli, kulipia gharama za uendeshaji na
kutekeleza matengenezo makubwa.

“Kisheria na kimkataba, DAWASA ina wajibu wa kuisimamia DAWASCO ambayo imeingia nayo mkataba...kwa kuwa zote ni taasisi na mashirika ya umma ambayo bodi na watendaji wake wakuu huteuliwa na mamlaka zile zile na kuripoti kwa watu
wale wale, hali hiyo ina athari katika utendaji na uwajibikaji.

“Umefika wakati wa mkataba kati ya DAWASA na DAWASCO, kuwekwa wazi kwa umma, kufanyiwa tathmini ya miaka zaidi ya mitano iliyopita ya utekelezaji, marekebisho kwa ajili ya kipindi kilichobaki na maandalizi mfumo bora unaopaswa kuandaliwa
baada ya kuisha mkataba huo mwaka 2015,” alisema.


Alisema wakazi wengi wa Dar es Salaam hasa wenye mabomba yanayojulikana kama ya wachina, kwa muda mrefu hayatoi maji
na wengine, maeneo wanayoishi hayana miundombinu ya maji
hivyo Serikali inapaswa kuchukua hatua za haraka ili kutekeleza
msingi wa hoja binafsi aliyoiwasilisha bungeni.

Bw. Mnyika aliwalalamikia Naibu Spika wa Bunge (Job Ndugai), Katibu wa Bunge (Dkt. Thomas Kashililah na Ofisi ya Bunge kwa kukwepa kumpa nakala za kumbukumbu za Bunge (Hansard) zinazohusu vikao husika.

“Tangu nilieleze Bunge kusudio langu la kukata rufaa dhidi ya ukiukwaji wa kanuni uliofanywa kuhusu hoja binafsi, hadi sasa naendelea kuzungushwa...Februari 13 mwaka huu, Dkt. Kashililah alidai uamuzi wa kuondolewa hoja yangu si ukiukwaji wa kanuni.

No comments:

Post a Comment