11 February 2013

Msako walioficha fedha nje waanza *JK aridhia kuundwa kwa Kamati Maalumu *Pinda awaonya viongozi wa dini, wanasiasa



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imeanza kufanyia kazi hoja binafsi ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe ambaye Novemba 9,2012, alilitaka Bunge lipitishe azimio namba 9/2012 la kuitaka Serikali ichukue hatua dhidi ya Watanzania walioficha fedha haramu
nje ya nchi.


Akisoma hotuba ya kuhitimisha Bunge la 10 mjini Dodoma jana, Waziri Mkuu, Bw. Mizengo Pinda, alisema Rais Jakaya Kikwete ameridhia kuundwa kwa Kamati Maalumu ya Kitaifa kushughulia hoja hiyo ambayo inaratibiwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali
(AG), Jaji Frederick Werema.

Alisema kamati hiyo inaundwa na wajumbe wanane wanaotoka katika Taasisi za Kitengo cha Kudhibiti Fedha Haramu, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini (TAKUKURU), Jeshi la Polisi, Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Usalama wa Taifa na Ofisi
ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali.

“Rais Kikwete aliridhia kuundwa kwa kamati hii Desemba 31,2012
ambayo kazi zake ni kuchunguza na kubaini majina ya Watanzania wanaodaiwa kuficha fedha nje ya nchi kinyume na Sheria na Kanuni za Nchi, kuchunguza iwapo fedha hizo ni haramu au la, kuzitambua benki na nchi ambazo fedha hizi zimefichwa.

“Majukumu mengine ya kamati ni kuandaa mashtaka dhidi ya Watanzania watakaobainika kuficha fedha hizi na kuishauri
Serikali jinsi ya kuzuia uhalifu wa makosa ya fedha,” alisema.

Bw. Pinda aliongeza kuwa, kamati hiyo imeanza kazi Januari 9 mwaka huu, kwa kupanga namna ya kutekeleza kazi zake hususan kukusanya taarifa kuhusu Watanzania wanaodaiwa kutorosha fedha hizo na kuangalia namna ya kupata taarifa muhimu nje ya nchi.

Alisema ili kuiwezesha kamati hiyo ifanye kazi zake kwa ufanisi mkubwa, wajumbe wake wanahitaji kupewa ushirikiano mkubwa
wa wananchi kwa kutoa taarifa mbalimbali kuhusu suala hilo.

“Natoa wito kwa Wananchi wote wenye taarifa sahihi zinazoweza kuisaidia Kamati kutekeleza kazi hii, wajitokeze kutoa maoni yao kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, waheshimiwa wabunge pia nawaomba mtoe ushirikiano,” alisema.

Aliongeza kuwa, katika azimio namba 9/2012, pamoja na mambo mengine liliitaka Serikali iwasiliane na Benki ya Dunia kupitia Kitengo cha Asset Recovery Unit ili mabilioni ya fedha ambazo zinamilikiwa na Watanzania katika benki za nje zirudishwe.

Alisema fedha hizo hufichwa ili kukwepa kulipa kodi ambapo Watanzania wote wenye akaunti za fedha nje ya nchi, waeleze wamezipataje ili TAKUKURU iweze kuchukua hatua.

“Hoja hii iliazimiwa na Bunge ambapo Serikali iliahidi kuleta taarifa ya hatua iliyochukuliwa ili kuziba mianya ya utoroshaji wa fedha nje ya nchi,” alisema Bw. Pinda.

Umoja wa kitaifa

Katika hatua nyingine, Bw. Pinda alisema kuwa, hivi karibuni kumeibuka dalili za kupoteza sifa yetu nzuri ya Umoja wa Kitaifa
na amani iliyodumu kwa miaka mingi nchini.

Alisema inasikitisha kuona vyama vya siasa vikionesha dalili ya kuhamasisha wanachama wao kuingia kwenye  malumbano ya 
siasa wenyewe kwa wenyewe au chama kingine.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa nchini, kuepuka kutumia majukwaa ya siasa kuvuruga amani, utulivu uliopo, kuepuka kutoa matamko ya vitisho, kuhamasisha wanachama wao kuendeleza vitendo vya uvunjifu wa amani, kujenga chuki na uhasama
miongoni mwa jamii kwa Serikali iliyopo madarakani.

Aliongeza kuwa, pamoja na kutofautiana kwa mawazo na sera za vyama hivyo ni muhimu tujenge mazingira ya kuvumiliana kwa
hali ya juu ili kuimarisha demokrasia ya kweli nchini.

Alisema viongozi wa vyama wanatakiwa kueleza sera zao badala ya kutukanana, kubezana, kushutumiana na kuzomeana ili kujenga nchi ya amani na kuchochea maendeleo endelevu.

“Tumeshuhudia pia kuibuka kwa choko choko za kidini, baadhi ya waumini wamekuwa wakikashifu dini nyingine kwa kejeli na vitendo vingine visivyostahili.

“Baadhi ya viongozi wa madhehebu ya dini wamekuwa wakiwaingiza waumini wao katika migogoro isiyoisha,
kufungiana milango na kuzuia waumini wasiabudu siku
za ibada...napenda kusisitiza kuwa, madhehebu ya dini
yana nafasi kubwa ya kujenga umoja wa kitaifa, amani
na mshikamano,” alisema.

Aliwaomba viongozi hao kutatua kwa amani migogoro iliyopo na kuelimisha waumini wao kuthamini, kujenga na kuenzi amani iliyopo nchini kwani Serikali imetoa uhuru wa wananchi wake Kuabudu, kila mtu kwa dini anayoitaka.

Hali ya chakula nchini

Bw. Pinda aliongeza kuwa, tathmini iliyofanyika hivi karibuni juu
ya upatikanaji wa chakula nchini na athari za mvua zinazoendelea kunyesha, inaonesha maeneo mengi hasa yanayopata mvua za msimu, mazao mengi yapo katika hatua za ukuaji.

Mikoa hiyo ni Mbeya, Ruvuma, Rukwa, Iringa, Tabora na Mtwara ambapo matarajio ni kwamba, kama mvua hizo zitaendelea vizuri,  upatikanaji chakula katika maeneo hayo utakuwa mzuri.

Alisema tathmini ya hali ya chakula na lishe iliyofanyika Januari mwaka huu, inaonesha kuwepo upungufu wa chakula katika Wilaya 47 zilizoko katika mikoa 15, ambazo zitahitaji msaada wa chakula katika vipindi tofauti.

Inakadiriwa kuwa, watu 1,615,445 watahitaji tani 32,870 za chakula hivyo Serikali itahakikisha Kitengo cha Hifadhi ya Taifa ya Chakula (NFRA), kinaendelea kusambaza mahindi katika maeneo yenye uhaba wa chakula.

“Hadi sasa tani 20,000 zilimetolewa katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara, Dodoma, Singida, Morogoro, Lindi, Tanga, Mtwara, Pwani, Dar es Salaam, Mwanza, Shinyanga, Simiyu, Mara na Tabora,” alisema Bw. Pinda.


Mchakato wa Katiba Mpya

Alisema Tume ya Mabadiliko ya Katiba imemaliza kukusanya maoni binafsi ya wananchi mmoja mmoja kama mchango wao
kwa ajili ya kuandika Katiba Mpya.

Aliongeza kuwa, hivi sasa tume inaendelea na kazi za uchambuzi wa maoni yaliyotolewa na wananchi pamoja na makundi maalumu ili baadaye kuandaa Rasimu  ya Katiba ambayo itawasilishwa katika Mabaraza ya Katiba yatakayoitishwa na tume nchini kote.

Mikutano ya Mabaraza ya Katiba itaanza Juni mwaka huu kwa kujumuisha wajumbe watakaochaguliwa na wananchi wenyewe kuanzia ngazi ya Kijiji. Wajumbe hao watapaswa kuwasilisha
maoni ya wananchi katika mikutano hiyo.

Kwa mujibu wa rasimu hiyo, katika Mikoa ya Tanzania Bara ukiondoa Dar es Salaam, kila Kata itawakilishwa na wajumbe
wanne watakaochaguliwa kutoka miongoni mwa wakazi wa
vijiji vilivyopo kwenye kata wakiungana na madiwani wao
pamoja na wale wa Viti Maalumu.

Wajumbe hao wataunda Baraza la Katiba la Wilaya ambapo kwa Mkoa wa Dar es Salaam, tume imeandaa utaratibu tofauti wa kuwapata wajumbe hao ambapo kila kata watatoka wajumbe
wanane ambao wataungana na Madiwani wa Kata na Madiwani wa Viti Maalumu hivyo kupata wajumbe 18,169 ambao watahudhuria mabaraza hayo ngazi ya Wilaya.

Upande wa Zanzibar, kutakuwa na Mabaraza ya Katiba ya
Wilaya Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa 13 ambapo
kila Shehia itawakilishwa na wajumbe watatu (3).

Wajumbe hao wataungana na madiwani wa wadi, madiwani wa Viti Maalumu na madiwani wa kuteuliwa waliopo kazini kwa sasa hivyo wajumbe wote wa Mabaraza ya Katiba watakuwa 1,198.

Bw. Pinda aliahirisha Bunge hilo hadi Aprili 9 mwaka huu saa tatuy asubuhi.

Mwisho.

No comments:

Post a Comment