11 February 2013
Askofu Laizer kuzikwa Febr. 15 *JK atuma salamu kwa Malasusa, Bunge lamlilia
Na Gladness Mboma
ALIYEKUWA Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Kati, Thomas Laizer, aliyefariki
juzi mjini Arusha, wakati akipatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Selian mjini humo, atazikwa Februari 15 mwaka huu.
Askofu Mkuu wa kanisa hilo, Dkt. Alex Malasusa, aliyasema hayo mjini humo jana wakati akielezea wasifu wa marehemu na taratibu
za mazishi kwa waandishi wa habari.
Alisema kanisa hilo, waumini wake na Watanzania kwa ujumla wameshtushwa na kifo cha Askofu Laizer ambaye ataendelea kukumbukwa kwa ujasiri aliokuwa nao na ushupavu wake
katika masuala mbalimbali kijamii nchini.
“Askofu Laizer alianzisha miradi mingi ya maendeleo ambayo inawasaidia sana waumini wa kanisa hili na jamii ambayo
imeweza kuondokana na umaskini na kujiletea maendeleo.
“Kabla ya kifo chake, Askofu Laizer alipatiwa matibabu ndani
na nje ya nchi ambapo kanisa kwa kushirikiana na familia yake,
tunashirikiana kuandaa taratibu za mazishi,” alisema.
Aliongeza kuwa, mazishi hayo yatafanyika katika Katika Kuu la
KKKT Mjini Kati Arusha ambapo waumini na Watanzania kwa
ujumla, watapata fursa ya kutoa heshima za mwisho Februari 14
mwaka huu katika Kanisa la Dayosisi ya Kaskazini Kati.
“Baada ya kutoa heshima za mwisho, mwili wa Askofu Laizer utapelekwa katika Kanisa Kuu Mjini Kati kwa ajili ya ibada
maalumu ya mazishi Februari 15 mwaaka huu,” alisema.
Dkt. Malasusa alisema marehemu alizaliwa Machi 10,1945 katika Wilaya ya Arumeru, mkoani Arusha, alisoma Shule ya Msingi Longido na mwaka 1965, alihitimu Elimu ya Juu katika masomo
ya Sosholojia kwenye Chuo cha Makumira mjini Arusha ambapo
baadaye alisomea Shahada ya Juu nchini Marekani.
Katika hatua nyingine, Bunge limetoa salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Askofu Laizer ambacho ni pigo kwa
waumini wa dini hiyo na Watanzania kwa ujumla.
Salumu hizo za rambirambi zimetolewa bungeni mjini Dodoma
jana na Mwenyekiti wa Bunge, Bi. Jenista Mhagama ambaye pia
ni mbunge wa Peramiho, mkoani Ruvuma, alisema Bunge hilo linaungana na waumini wa madhehebu yote nchini kuomboleza
msiba wa kiongozi huyo wa kanisa.
Wakati huo huo, Rais Jakaya Kikwete ametuma salamu za rambirambi kwa Dkt. Malasusa ili kuomboleza kifio cha
Askofu Laizer.
Alisema taarifa za msiba huo amezipokea kwa mshtuko mkubwa
na ataendelea kukumbukwa kama kiongozi aliyetumia vipaji vyake
kuwahudumia waumini na Watanzania wote.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment