06 February 2013

Mradi wa 'Niache Nisome' usambazwe nchi nzima


Na Rose Itono

WIZARA ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi imekabidhiwa majukumu ya kuweka viwango vya ubora wa elimu na mafunzo ya ufundi katika ngazi zote za elimu kuanzia awali mpaka sekondari.

Sambamba na hilo wizara pia ina wajibu wa kuhakikisha kuwa elimu ya awali,msingi,sekondari na ile ya watu wazima inatolewa kwa kuzingatia viwango vinavyokubalika.

Wizara pia ina jukumu la kusimamia utekelezaji wa utoaji wa elimu kwa kufanya ufuatiliaji na tathmini pamoja na kufanya mapitio,kuandaa na kutoa mapendekezo ya marekebisho ya Sera, Mipango, Sheria na kanuni za elimu zilizopo,kulingana na mabadiliko ya dhima na dira ya Serikali huku ikiandaa mikakati ya utekelezaji wake.

Aidha, Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ndiye msimamizi mkuu wa masuala ya taaluma katika ngazi zote za elimu na mafunzo.

Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi inatekeleza mipango mbalimbali ili kuinua ubora wa elimu

Ili yote hayo yaweze kufanikiwa juhudi za wazazi na walezi kwa kushirikiana na wanafunzi zinahitajika kwa kiasi kikubwa katika kuleta matokeo mazuri.

Nimeongea hivyo kwa makusudi kwani kumekuwa na baadhi ya wazazi,walezi ambao wamekuwa wakiwakatisha masomo wanafunzi hasa wa kike kwa kutaka kuwaoza kwa nguvu kwa nia ya kujipatia fedha ama mali.

Nionavyo hii ni ukiukwaji wa haki za binadamu kwa kumyima haki yake ya msingi ya kupata elimu mtoto wa kile na kumjengea .

Kutokana na hali hiyo ipo haja ya serikali kuianzia ngazi zake za mtaa kuielimisha jamii matatizo na madhara ya watoto wa kike kuolewa kabla ya umri wao na umuhimu wa watoto kusoma.

Nionavyo kwa kufanya hivyo kutalipunguza tatizo la wazazi ambao wana tamaa za kujipatia pesa kwa mahari kupitia watoto wao bila kuangalia madhara na vitu vya msingi ambavyo mtoto wa kike atavikosa kutokana na kuolewa bila kuwa na elimu.

Hivi karibuni tumeshuhudia mtoto wa kike ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili katika shule ya sekondari Tongani kata ya Mkaramo wilayani Pangani akitoroka kwao na kukimbilia kujificha porini akikwepa kuachishwa shule.

Nionavyo hali hii ni hatari kiusalama kwa mtoto huyo ambaye angeweza kupata madhara ya kukutana na wanyama wakali na hata kupoteza maisha.

Hali ya mtoto huyo kuamua kulala porini ilimuwezesha kufika kwa Mkuu wa Wilaya ya handeni kuomba msaada ambao utamuwezesha kuweza kuendelea na masomo.

Nionavyo kulingana na hali hiyo ni wanafunzi wangapi wenye ujasiri kama aliouonyesha msichana huyo ambaye aliamua kujitoa muhanga na kuamua kulala porini ili kukimbia kuolewa.

Kwa maelezo ya mtoto huyo anasema aliamua kukimbilia kwa Mkuu wa Wilaya baada ya kusikia kuwa kuna mradi wa 'Niache Nisome' ambao umeanzishwa kwa ajili ya kumkomboa mtoto wa kike dhidi ya mimba na ndoa za utotoni.

Nionavyo kwa mfano wa mradi huu ni wazi serikali ikaona umuhimu wa mradi huo kusambaa nchi nzima ili kuwawezesha vijana wa kike kujikomboa na ndoa na mimba za utotoni.

No comments:

Post a Comment