06 February 2013

Wapema mafunzo kupunguza viwavi jeshi



Na Mariam Mziwanda

MAOFISA Kilimo zaidi ya 20 kutoka Wilaya tano nchini, wapo kwenye mafunzo ya mradi shirikishi wa kupunguza wimbi la
viwavi jeshi ambavyo ni kero sugu kwa wakulima na kusababisha njaa katika baadhi ya maeneo nchini.

Akizungumza katika mafunzo hayo Dar es Salaam juzi, mwezeshaji wa mafunzo hayo ambaye pia ni Ofisa Kilimo kutoka Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, Kanda ya Kaskazini, Bw. Didas
Moshi alisema mafunzo hayo yatawasaidia maofisa hao
kuwatambua na kuwaangamiza kabla ya kukua.

“Tumeanza mafunzo haya na Wilaya tano ambazo ni Kisarawe, Nachingwea, Masasi, Lindi Vijijini na Kilwa, mafunzo haya yanaendeshwa kwa msaada wa watu wa Marekani ambao
wameona viwavi jeshi ni kero kwa wakulima,” alisema.

Akifungua mafunzo hayo, Mkurugenzi Msaidizi wa Afya ya Mimea kutoka katika Wizara hiyo, Cornelius Mkondo, alisema mazao mengi ya wakulima nchini yamekuwa yakiathiriwa na milipuko
ya wadudu sugu wanaoshambulia mazao kwa haraka.

Alisema viwavi jeshi wamekuwa wakipoteza nguvu kazi za wakulima hivyo imeamua kutafuta mbinu za kuwatokomeza.

Aliongeza kuwa, maofisa hao watafundishwa mambo mengi hususan jinsi ya kufahamu mlipuko unavyotokea na kuimarisha mawasiliano kati ya vijiji, kata, Wilaya hadi Taifa.

“Lengo ni kujilinda na viwavi, katika kuhakikisha operesheni hii inakuwa endelevu, tutashirikiana na kampuni za simu ili wakulima waweze kufahamu utabiri wa hawa wadudu waharibifu,” alisema
na kuongeza kuwa, mradi huo mbali ya Tanzania pia unaendeshwa katika nchi za Kenya na Ethiopia.

No comments:

Post a Comment