05 February 2013

Moravian lawaonya wachungaji



Na Charles Mwakipesile,  Mbeya

KANISA la Moravian nchini, limewaonya wachungaji wanaodaiwa kutumiwa na wanasiasa ili kuanzisha migogoro katika kanisa hilo ambayo inakiuka katiba, kuvuruga amani na utulivu.


Ili kukomesha vitendo hivyo, kanisa hilo limeazimia kuhakikisha wachungaji wote wanaotumika kisiasa, wanafukuzwa haraka iwezekanavyo ili wasiendelee kuleta mpasuko zaidi.

Katibu Mkuu wa kanisa hilo nchini,  Mchungaji Conrad Nguvumali, aliyasema hayo mjini Mbeya jana wakati akizungumzia mgogoro uliolikumba Jimbo la Kusini, Misheni ya Dar es Salaam.

Aliunga mkono hatua ya kufukuzwa baadhi ya wachungaji waliobainika kupeleka siasa katika kanisa hilo.

Alisema hakuna Mchungaji wa kanisa hilo anayedai kuwa na mali badala yake mali zote zipo chini ya jimbo mama hivyo kitendo walichotaka kufanya baadhi ya wachungaji wa Dar es Salaam
ni kinyume na taratibu na kinapaswa kukemewa.

“Ni hatari kubwa kwa wachungaji kuanzisha migawanyiko kwenye kanisa kwani si kiapo chao bali waliapa kutumika mahali popote na yanapotokea mabadiliko, Mchungaji anapaswa kukubaliana nayo tofauti na kilichotokea katika Jimbo la Misheni.


“Kitendo cha kufunga Kanisa la Tabata, Dar es Salaa, hakiwezi kuvumiliwa kutokana na roho za waumini wengi kuumia kwa kukosa ibada baada ya kukuta milango imefungwa, walinzi na
polisi wakiwa wamezunguka eneo la kanisa,” alisema.

Aliutaka uongozi wa Kanisa hilo Jimbo la Kusini, ukiongozwa na Mwenyekiti wake, Mchungaji Clement Mwaitebele, kuhakikisha unaendelea na jitihada za kufuata taratibu ili amani na utulivu viendelee  kuwepo katika eneo hilo.

No comments:

Post a Comment