05 February 2013

Warioba: Tumeanza kuchambua maoni



Na Darlin Said

TUME ya Mabadiliko ya Katiba, imeanza kuchambua maoni
ya wadau ili kuandaa rasimu ya kwanza ya Katiba ambayo itawasilishwa katika Mabaraza ya Katiba yatakayoanza
kuijadili rasimu hiyo kuanzia Juni mwaka huu ili kutoa
maoni ya kuiboresha.


Mwenyekiti wa tume hiyo, Jaji mstaafu Joseph Warioba, aliyasema hayo Dar es Salaam jana wakati akitoa tathmini ya ukusanyaji maoni ya Katiba Mpya kutoka kwa makundi maalumu na watu mashuhuri wakiwemo viongozi wastaafu na waliopo madarakani.

Alisema rasimu mpya ya kwanza ambayo itaandaliwa, itachapishwa katika magazeti kwa mujibu wa Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ili wananchi waisome kabla ya kuwasilishwa rasmi katika Mabaraza ya Katiba, ngazi ya Wilaya.

Alifafanua kuwa, muundo wa mabaraza hayo kila kata itakuwa na wajumbe watano ambao mmoja ni diwani wa kata husika, wanne watachaguliwa na wananchi kuanzia ngazi ya kijiji.

Alisema kwa upande wa mikoani, kila Wilaya itakuwa na baraza moja ambalo wajumbe wake watatoka katika kata husika pamoja
na madiwani wao.

Jaji Warioba alisema utaratibu huo utakuwa tofauti jijini Dar es Salaam ambapo kila kata itakuwa na wajumbe wanane na Wilaya tatu za jiji hilo, Ilala, Kinondoni na Temeke, kila moja itakuwa
na mabaraza mawili.

“Tumeamua kuongeza idadi ya mabaraza jijini Dar es Salaam kutokana na wingi wa watu waliopo ili kuwapa nafasi wananchi waweze kutoa maoni yao kupitia wajumbe waliowachagua,”
alisema Jaji Warioba.

Aliongeza kuwa, tume hiyo imeshatoa miongozo mbalimbali, sifa
za waombaji wa nafasi ya ujumbe wa mabaraza hayo pamoja na utaratibu wa kuwasilisha maombi yao.

Wakati huo huo, Jaji Warioba alisema rasimu hiyo pia itapelekwa kwa makundi mbalimbali kama vyama vya siasa, taasisi za dini, Serikali na makundi mengine yaliyotoa maoni kwa tume na yasiyobahatika kutoa maoni yao ili waweze kuijadili.

Awali alisema katika ukusanyaji maoni wa makundi, ushirikiano ulikuwa mzuri ambapo jumla ya makundi 170 yalitoa maoni yao.

Makundi yaliyotoa maoni hayo ni asasi 22 za dini, kiraia 72, taasisi za Serikali 71, vyama vya siasa 19, viongozi na watu mashuhuri 43 kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

No comments:

Post a Comment